Na: Lilian Lundo – MAELEZO
Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia inaukumbusha Umma kuwa mitihani ya Taifa ya Darasa la 4 na
Kidato cha 2 itaendelea kuwepo na mwaka huu itafanyika kama kawaida.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
Dkt. Leonard Akwilapo ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa
akikanusha taarifa za kutokuwepo kwa mitihani hiyo kwa mwaka 2016.
“Napenda niukumbushe Umma kuwa
mitihani hii ni muhimu sana katika ufuatiliji wa maendeleo ya wanafunzi
wetu. Kwa hiyo mitihani yote miwili itaendelea kuwepo na mwaka huu
itafanyika kama kawaida. Kama kuna watu wanawaambia kuwa haitafanyika
wawapuuze kabisa,” alifafanua Dkt. Akwilapo
Dkt. Akwilapo aliendelea kwa
kusema kuwa, mitihani hiyo ina umuhimu mkubwa katika kupima maendeleo ya
mwanafunzi kwa lengo la kufanya maendeleo ya kitaaluma. Aidha kwa
wanafunzi ambao watakuwa hawajafikia viwango vya ufaulu vilivyowekwa
watatakiwa kukariri darasa au kidato.
Amebainisha kuwa Baraza la
Mitihani ndilo lenye jukumu la kushughulikia maandalizi ya mitihani hiyo
ikiwa ni pamoja na utungaji, uchapaji, ufungaji na usafirishaji hadi
ngazi ya Mkoa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(OR-TAMISEMI) ikiwa na majukumu ya kuhakikisha kuwa uendeshaji na
usahihishaji wa mitihani hiyo unafanyika kikamilifu.
0 maoni:
Chapisha Maoni