Katibu wa Chama cha Waigizaji cha
Mkoa wa Kinondoni (STDFAA) , Jafari Makatu akiongea na waandishi wa
habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam juu ya changamoto
zinazowakabili katika tasnia ya filamu nchini, kulia ni Mwenyekiti wa
chama hicho, Ali Baucha na kushoto ni Mdhamini wa Chama hicho, Ahmed
Olotu.
……………………………………………………………………………
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Chama cha Waigizaji cha Mkoa wa
Kinondoni (STDFAA) wamemuomba Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mhe Nape Nnauye kuiharakisha Sera ya filamu ili iwasaidie
katika mambo mbalimbali hususani ya kisheria.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Katibu wa Chama hicho, Jafari Makatu alipokuwa akiongea na
waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya
Tano pamoja na kuzungumzia changamoto zinazowakabili katika tasnia ya
filamu nchini.
Makatu amesema kuwa Sheria ya
Filamu ni muhimu katika tasnia hiyo hivyo ikiharakishwa itasaidia wadau
wa tasnia hiyo kufanya kazi kwa uwazi na usalama wa hali ya juu kwa kuwa
watakua wanalindwa na sheria.
“Tunamuomba Waziri wetu Mhe. Nape
atuharakishie Sera ya Filamu kwa sababu sheria hiyo itatusaidia
kuoanisha mambo mbalimbali ya kisheria kuanzia kwenye uandaaji wa kazi
zetu hivyo, kupelekea kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa kazi bora
zaidi”. Alisema Makatu.
Ameongeza kuwa sheria hiyo pia
itawasaidia katika suala zima la Haki miliki na Haki shiriki, malipo
stahiki kwa kila kazi, masoko, madaraja ya waigizaji na wadau wote wa
tasnia ya filamu pamoja na ulazima wa kila msanii kujiunga katika vyama
husika vitakavyowasaidia katika mambo mbalimbali.
Aidha, Katibu huyo ameiomba
Serikali kuwekeza kwenye sanaa ili kuwawezesha kuifanya kazi hiyo kwa
ufanisi na kuchangia katika Pato la Taifa pia amemuomba Mhe.Nape
kuwatafutia eneo maalum la ardhi ambalo litawasaidia katika kufanyia
shuhuli zao za kurekodi filamu.
Ametoa rai kwa wasanii kujiunga
katika vyama mbalimbali vinavyowahusu ili kuleta umoja, mshikamano na
tija katika kazi za sanaa,amesisitiza wasanii kujiunga na Bima za Afya.
Naye Mdhamini wa Chama hicho,
Ahmed Olotu amewaomba waandishi wa habari kutumia kalamu zao katika
kuwasaidia wasanii kupambana na wauzaji wa filamu feki kwa kuwa
wanarudisha nyuma maendeleo ya wasanii na kupunguza pato la Taifa.
0 maoni:
Chapisha Maoni