Postedy by Esta Malibiche on August 2016
Meatu,Simiyu
Waganga wakuu wa mikoa na wilaya
wote nchini wametakiwa kuwa na vyumba vya upasuaji ‘theate’ zenye
kufanya kazi ipasavyo kwenye vituo vyote vya afya kwenye maeneo yao
ndani ya miezi 6.
Agizo hilo limetolewa na Naibu
waziri wa Afya,maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Hamis
Kigwangwalla mara baada ya kutembelea kituo cha afya cha Mwandoya
kilichopo Meatu mkoani Simiyu kilichopo umbali wa kilometa 60 kutoka
hospitali ya wilaya ya meatu
“Hawa wa Meatu wenyewe wana kituo
cha Afya Mwandoya wamekipa uwezo wa kufanya upasuaji kituo
hiki,Wamenunua vifaa, wameajiri hadi Daktari (MD) kwa ajira ya muda kwa
ajili ya kufanya kazi pale”.
Aidha, alisema Kituo hicho
kimefanya takriban operation 40, zote salama Kwa asilimia 100.
Wamepunguza msongamano Mwanhuzi na wamepeleka huduma nyeti na za kuokoa
maisha Karibu zaidi na wananchi, ukizingatia huku hakuna barabara za
lami na hakuna gari la kubebea wagonjwa (ambulances).
“Leo nimeamua kuchukua uamuzi wa
kutoa agizo kali kabisa toka nimeteuliwa. Najua litazua maswali, lakini
litaokoa maisha ya wanawake wajawazito wa nchi yetu (CEmOC) na wananchi
wengine, Nitalitetea. Nitalisimamia”alisisitiza dkt.Kigwangwalla.
“Wiki iliyopita nilitembelea
Manispaa ya Ilala, kwenye vituo vya afya vitatu nilivyotembelea hakukuwa
na theatre yenye kufanya kazi. Kwa mujibu wa sera ya afya ya Tanzania,
‘kituo cha afya’ kitakuwa na hadhi hiyo kama kina uwezo wa kufanya
upasuaji. Vinginevyo hiyo ni zahanati. Mara nyingi watendaji hawa
wamekuwa wakijificha kwenye kichaka cha ‘hatuna fedha’, wengine wakiomba
fedha kutoka serikali kuu”.
Hata hivyo alimuuliza Mkurugenzi wa Ilala, anakusanya
shilingi ngapi Kwa mwezi, akasema bilioni 6. Nikamuuliza unadhani ni
shilingi ngapi kuwa na theatre yenye kufanya kazi? Akakosa jibu. Nikampa
miezi 6 awe na theatre zenye kufanya upasuaji. Naibu waziri huyo anasema jana ametembeleaMkoa wa Shinyanga na Simiyu na kukutana na tatizo hilo hilo alipokuwa Kishapu, Shinyanga na Mwanhuzi, Simiyu.
“Nimesema sababu za kuwa Halmashauri hazina pesa huku zinakusanya mamilioni ambayo wanayatumia bila kuainisha matatizo ya msingi ya wananchi hazikubaliki, Leo iwe mwisho”. Nawaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini washirikiane na Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya wajue watakavyofanya wahakikishe wanafungua huduma za upasuaji kwenye vituo vyote vya afya nchini ndani ya miezi sita (6).
“Baada ya miezi hiyo sita mimi mwenyewe na timu yangu ya kurugenzi ya ukaguzi na uhakiki ubora wa huduma za afya (inspectorate and quality assurance) tutasambaa nchi nzima kukagua huduma hizi na pale ambapo hatutozikuta tutakishusha hadhi kituo hicho kutoka ngazi ya ‘kituo cha afya’ na kuwa ngazi ya ‘zahanati’ sambamba na kuwashauri wenzetu wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwa wakuu hao wa idara wameshindwa kutekeleza majukumu yao na hivyo wawashushe vyeo”. “Nitasimamia uamuzi huu Kwa nguvu zangu zote. Sababu ni kwamba ninajua faida yake. Ninajua Mungu atafurahi, atanibariki”.
Wakati wa Bunge la bajeti wanaharakati wa haki za wanawake na Watoto waliwahamasisha Wabunge wawashughulikie Kwa ajili ya suala hili. Wakawa washawishi wabunge kuwa kwa siku takwimu za vifo vinavyotokana na sababu za uzazi ni sawa na ‘coaster’ moja ipate ajali na iue watu wote! Wabunge waligeuka mbogo. Japokuwa namba hizi zilikuwa zilizidishwa, walifikisha ujumbe kwetu mawaziri. Kwamba lazima tufanye kitu tofauti kwenye eneo hili. Mimi naanza kuchukua hatua. Vifo vitokanavyo na uzazi havikubaliki! Alisema Naibu waziri wa afya.
0 maoni:
Chapisha Maoni