Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kupitia kikosi cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha limekamata watu wanne kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi wa kanda hiyo, Hezron Gymbi amesema watuhumiwa hao walikamatwa jana maeneo ya Chamanzi muda mfupi baada ya kukutana na kupanga kufanya uhalifu wa kutumia silaha.
Watuhumiwa hao wanaofahamika kwa majina ya Uswege Seleman (23), Hassan Abdallah (73), Said Kiwambu (39) na Hamadi Badrilu (28) walikutwa na silaha aina ya MARK 4 yenye namba LA-227725A baada ya askari polisi kufanya upekuzi katika nyumba waliyokutana.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumefuatia baada ya raia mwema kutoa taarifa kwamba kuna watu wanaoshukiwa kuwa majambazi wanaotumia silaha katika matukio mbalimbali kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga na Lindi.
Na Regina Mkonde