Mwashamu
Askofu wa Jimbo Katoliki la Mtwara akikata keki wakati wa sherehe za
kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini
Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda, katikati ni Mkurugenzi wa Redio
Maria Tanzania (RMTZ) Padre John Maendeleo.
Spika
Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda
akikata keki wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya
Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam yaliyoanza rasmi tangu
April 26 mwaka huu. Katikati ni Mwashamu Baba Askofu wa Jimbo Katoliki
la Mtwara Titus Mdoe,kutoka kulia ni Mhamasishaji Mkuu wa Redio Maria
Tanzania Bi. Veronica Mwita na wapili kushoto ni Mkurugenzi wa Redio
Maria Tanzania (RMTZ) Padre John Maendeleo.
Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Benjamin William Mkapa akisalimiana na Baba Askofu wa Jimbo
Katoliki la Mtwara Mwashamu Askofu Titus Mdoe wakati wa sherehe za
maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es
Salaam.Katikati ni Mkurugenzi wa Redio Maria Tanzania Padre. John
Maendeleo.
Askofu
Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Saalam Mwadhama Polycarp Kardinali
Pengo akizungumza na wadau na marafiki wa Redio Maria Tanzania leo
Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 20 tokea
kuanzishwa kwa Redio hiyo
Mkurugenzi
wa Redio Maria Tanzania Padre John Maendeleo akizungumza na wadau na
marafiki wa Radio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam wakati wa
hafla ya kuadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwa Redio hiyo.
Rais
wa Redio Maria Tanzania Humphrey Julius Kira akizungumza na wadau na
marafiki wa Radio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam wakati wa
hafla ya kuadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwa Redio hiyo.
Spika
Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda
akipokea risala kutoka kwa Rais wa Redio Maria Tanzania Humphrey Julius
Kira(Kulia) wakati wa sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya
Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es Salaam.
Spika
Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda
akipeana mkono na baadhi ya marafiki wa Redio Maria Tanzania waliofika
kuchangia Redio hiyo katika harambee iliyofanyika ikiambatana na sherehe
za maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania leo Jijini Dar es
Salaam. Kushoto ni Rais wa Redio Maria Tanzania Bw. Humphrey Julius
Kira.
Baadhi ya waumini wa Roman Katoliki wakifurahi wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 20 ya Redio Maria Tanzania (RMTZ).
Picha zote na Frank Shija, MAELEZO.
………………………………………………………………………………………………………………………..
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Rais wa Redio Maria Tanzania, Humphrey Kira
ameiomba Serikali kurekebisha Sheria ya leseni ya redio za jamii ili
ziweze kuwa na vituo vingi vya kurushia matangazo yake.
Hayo yamesemwa leo na Rais huyo wakati
alipokuwa akisoma risala kwenye sherehe za kilele cha maadhimisho ya
miaka 20 ya redio hiyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Msimbazi Centre,
Jijini Dar es Salaam.
Kira amefafanua kuwa redio za kijamii hasa
zilizojikita katika nyanja za kiimani zinasaidia kufundisha maadili na
kufanya wananchi wakomae kiimani, hivyo angefurahi sana kuona redio za
aina hiyo zinapewa leseni za kurusha matangazo yake nchi nzima.
“Ndugu mgeni rasmi, redio yetu inakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ufinyu wa sehemu za usikivu
(coverage areas) ambapo tatizo hili linatokana na sheria ya leseni za
redio ambayo hairuhusu redio za aina hiyo kuwa na vituo zaidi ya kumi
nchini nzima, tunaomba serikali itusaidie kuiboresha sheria hii ili
tuongeze vituo vya matangazo ya dini”, alisema Kira.
Rais huyo ameongeza kuwa majimbo yote
yanahitaji kufikiwa na huduma za maombi, hivyo anawashauri wasikilizaji
wote kuendelea kuisikiliza redio hiyo kwa njia ya mitandao ikiwemo simu
za mkononi kwani hivi sasa huduma hiyo inapatika nchi nzima.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu
Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ametoa rai
kwa uongozi wa redio hiyo kutobadilisha maudhui wala kuweka vipindi
visivyokuwa vya dini ili iendelee kuunganisha familia na sio kuzigawa
familia.
“Tunasema kuwa redio Maria ni sauti ya
kikristu nyumbani mwako lakini mimi nasema ni sauti ya Mungu ndani ya
familia kwa kuwa inafanya kazi ya kuunganisha familia, vyombo vingine
vya habari vinafanya kazi kubwa ya kuigawa familia lakini Redio Maria ni
tofauti”, alisema Pengo.
Askofu Pengo amewashukuru wananchi wote
waliohudhuria kwenye maadhimisho hayo kwa kuwa kufanya hivyo ni njia
moja wapo ya kumuenzi na kumpa heshima Mama Bikira Maria.
Nchini Tanzania, Redio Maria ilianzishwa
Aprili 26 mwaka 1996 katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea ikiwa na lengo
la kumsaidia Mama Bikira Maria katika kazi yake ya kumtangaza Yesu
Kristo kwa watu wote. Mpaka sasa ina vituo 10 Tanzania Bara na viwili
Zanzibar.
0 maoni:
Chapisha Maoni