![]() | |
|
SERIKALI
iko katika hatua ya mwisho ya kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari (TPA) ambaye ni mtu sahihi na mwenye uwezo mkubwa
wa kusimamia na kuendesha bandari hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Kwa
mujibu wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa, tayari majina manne yameshawasilishwa na yanafanyiwa kazi ili
kuteua jina la mmoja atakayeteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA
Profesa
Mbarawa aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza mwishoni mwa
ziara yake ya siku mbili mkoani Kigoma, ambako alikutana na
wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena.
Akijibu
risala ya wafanyabiashara na wasafirishaji hao, Profesa Mbarawa aliitaka
TPA na Mamlaka ya Mapato (TRA) kufanya kazi siku za mwishoni mwa wiki
na sikukuu ili kuhudumia shehena za wafanyabiashara wanaotaka
kusafirisha mizigo yao kwenda nje ya nchi ili kuwafanya watumie siku
chache katika usafirishaji wa shehena zao.
Katika
risala yao, wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena walilalamikia
urasimu wa mamlaka hizo unaofanya wafanyabiashara kutumia siku nyingi
kusafirisha shehena zao na hivyo kusababisha kuwepo kwa ongezeko la
gharama katika usafirishaji wa shehena hizo wanapotumia Bandari ya
Kigoma.
Hata
hivyo, TPA katika warsha ya siku mbili kwa Wahariri wa Habari wa vyombo
mbalimbali nchini iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam,
ilisema bandari inafanya kazi saa 24 na kwamba kama nyaraka zote
zinazohitajika kutoa mzigo zinapatikana kwa muda mwafaka, mzigo
unatolewa ndani ya muda wa siku 0.2.
“Katika
ushindani wa biashara uliopo sasa baina yetu na wenzetu wa nchi nyingine
hatuna budi kufanya kazi kwa tija na ufanisi mkubwa ili kuwalinda
wateja wetu wasiweze kukimbia na kufanya kazi mwishoni mwa juma na siku
za sikukuu kama kuna shehena ya kupakia na kupakua bandarini ni jambo la
msingi sana katika kuwalinda wateja,” alisema Profesa Mbarawa.
Awali
akisoma risala ya wafanyabiashara na wasafirishaji wa shehena,
msafirishaji shehena kwenda nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Kassim Zaidi
alisema urasimu wa Kampuni ya Reli (TRL) kutumia siku nyingi
kusafirisha behewa zenye mzigo kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma na
urasimu wa TRA na TPA umewakimbiza wafanyabiashara na wasafirishaji
kutumia Bandari ya Kigoma na hivyo wengi wao kusafirisha shehena zao kwa
njia ya barabara.
Alisema
imekuwa ikichukua zaidi ya siku 15 kwa behewa zenye shehena kutoka Dar
es Salaam kufika Kigoma na wakati mwingine treni ikisimama njiani katika
baadhi ya mikoa kwa siku nyingi bila sababu yoyote hali ambayo imefanya
wasafirishaji wa shehena kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo
kutumia njia nyingine za usafirishaji kutumia barabara na bandari za
nchi nyingine kuepuka usumbufu.
Kwa
mujibu wa Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, hadi
kufikia Desemba mwaka jana, tani milioni 14.8 zilipita katika bandari
hiyo, lakini ni asilimia 0.01 pekee ndiyo zilizosafirishwa kwa njia ya
reli na asilimia 99.9 kwa barabara, kutokana na uchakavu wa reli na
usafiri wake kutokuwa wa kuaminika.
Naye
Zaidi alisema kwa waziri kuwa wamekuwa wakilalamikia vitendo vya baadhi
ya watumishi wa TRA na TPA kukataa kufanya kazi Jumamosi na Jumapili
wakitaka kulipwa posho ya kufanya kazi ya ziada na msafirishaji wa
shehena badala ya ofisi zao, hali aliyosema inawaingiza wasafirishaji
gharama kubwa za kuuhifadhi mzigo huo.







0 maoni:
Chapisha Maoni