Kampuni
ya kutengeneza vinywaji ya TBL Group iliyopo chini ya kampuni mama ya
kimataifa ya SABMiller imefanikiwa kutekeleza mpango wa uzalishaji
unaozingatia utunzaji wa mazingira na kunufaisha jamii zilizopo maeneo
ilipowekeza kwa kujenga viwanda vyake.
Hayo
yamebainishwa na Meneja wa kiwanda cha TBL cha Mwanza,Richmond Raymond
wakati akitoa mada kwenye semina kuhusu kujenga uchumi na maendeleo
endelevu iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Amesema
kwa muda mfupi wa utekelezaji wa mpango huo mafanikio yameanza kuonekana
na taasisi nyingi zinatembelea kwenye viwanda vyake kwa ajili ya
kujifunza.
Akitolea
mfano wa kiwanda cha Mwanza ambacho anakiongoza,Richmond alisema
uendeshaji wake unafuata mifumo bora na kuhakikisha jambo lolote
linalofanyika linaenda sambamba na malengo yaliyowekwa na kampuni mama
ya SABMiller ambayo mtazamo wake unaelekeza kwenye utunzaji wa
mazingira , kufanya uzalishaji usio na athari kwa mazingira na
kuhakikisha jamii zilizopo maeneo ya kiwanda zinanufaika na uwekezaji.
Richmond
alisema kiwanda cha Mwanza katika kuhakikisha uzalishaji wake
hauathiri mazingira kimefunga mitambo inayozalisha nishati ya umeme kwa
kutumia pumba za mpunga badala ya mafuta. “Uzalishaji huu mbali na
kupunguza gharama za uendeshaji pia umeongeza mapato ya wananchi ambao
wanauzia pumba za mchele kiwanda kwa ajili ya kuendeshea mitambo yake
wakati siku za nyuma walikuwa wanazitupa”.Alisema.
Pia
alisema TBL inahakikisha inapata malighafi kutoka kwa wazalishaji wa
ndani hususani wakulima wanaoiuzia malighafi ambapo inawawezesha kwa
kuwapatia mitaji na utaalamu wa kilimo ili waweze kupata mazao ya
kutosha ambayo wanayauza kwa kiwanda wakati huo huo kuboresha maisha
yao.
Alisema
mafanikio ambayo kampuni imepata na mikakati yake ya uwekezaji zaidi
nchini katika siku za usoni inazingatia zaidi malengo ya Kampuni ya
SABMiller yenye mwelekeo wa Maendeleo endelevu na kanuni za pamoja.
Meneja wa kiwanda cha TBL cha Mwanza,Richmond Raymond akitoa mada.
Richmond
aliyabainisha malengo hayo kuwa ni ‘dunia yenye nuru njema,lengo
hili limelenga kuharakisha ukuaji wa kampuni na maendeleo ya kijamii
katika mfululizo wake wa maadili.
Alilitaja
lengo lingine kuwa ni ‘kujenga dunia changamfu’ ambalo linalenga
kuifanya bia kuwa kinywaji cha asili kwa mnywaji na kuondoa dhana kuwa
unywaji wa bia ni ulevi, bali kuhamasisha unywaji ambao utawezesha
kuwepo wanywaji wa wastani kwenye jamii ambao pia watazingatia
kutekeleza majukumu yao.
Aidha
alilitaja lengo lingine kuwa ni ‘kujenga dunia imara na dunia iliyo
safi’ ambalo limelenga kupata raslimali ya pamoja ya maji ya kutosha
ambayo yanatumika kwa kiasi kikubwa katika biashara ya kampuni.”Katika
kutekelea lengo hili kampuni kwa muda mrefu imekuwa mstari wa mbele
kulinda na kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha maji yanayopatikana
yananufaisha jamii ya wananchi inayowazunguka”.
Lengo
lingine alilibainisha kuwa ni kujenga dunia yenye nguvu kazi lengo
kubwa likiwa ni kusaidia matumizi bora na endelevu ya ardhi .
Richmond
alisema malengo haya ambayo baadhi yake yanashabihiana na malengo
endelevu ya Umoja wa Mataifa yanadhihirisha kuwa kampuni ya TBL Group ni
kampuni iliyodhamiria kufanya uwekezaji wenye kuleta tija na mabadiliko
kwa jamii ya watanzania
0 maoni:
Chapisha Maoni