Mwenyekiti wa shirikisho la
waajiri la jumuiya ya Afrika Mashariki(EAEO),Rosemary Ssenabulya
akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha hivikaribuni kuhusu
mafanikio na changamoto za shirikisho hilo,kushoto kwake ni katibu wa
shirikisho hilo,Agrey Mlimuka na kulia kwake ni mkurugenzi mtendaji wa shirikisho la waajiri nchini Kenya,Jacqueline Mugo(Habari picha na Pamela Mollel wa jamiiblog)
……………………………………………………………………………………………………
Tanzania na Burundi
zimeombwa kulegeza misimamo yao kwa kuondoa gharama za vibali vya
kufanya kazi kwa raia wa nchi zinazounda jumuia ya Afrika Mashariki
(EAC) kama zilivyofanya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya ambazo nazo ni
wanachama wa jumuiya hiyo.
Akizungumza jijini Arusha
hivikaribuni Katibu wa Chama cha Waajiri Afrika Mashariki (EAEO), Aggrey
Mlinuka alisema kuwa hadi sasa nchi za Tanzania na Burundi ndizo nchi
pekee zilizobakia katika kutoza gharama za vibali vya wageni hasa raia
wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
Mlimuka alisema kuwa mbali
na nchi hizo kuondoa utaratibu huo pia amependekeza kwamba utaratibu wa
utoaji vibali hivyo usichukua muda mrefu kama ilivyo sasa kwa nchi za
Tanzania na Burundi na kushauri muda wa kuchukua vibali hivyo haustahili
kuzidi siku 30.
Katibu huyo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chama cha waajiri Tanzania (ATE) alisema kuwa chama chao
kiliwasilisha mapendekezo hayo mbele ya Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika
Mashariki, Dk. Richard Sezibera ambaye anamaliza muda wake April 20
mwaka huu.
“EAEO na Sezzibera
tumefanya kazi kubwa kuhakikisha jumuiya inasonga mbele kwa kasi kubwa
mbali na changamoto zilizopo katika nchi moja moja, lakini tuna uhakika
tutazitatua kwa manufaa na maslahi ya wana jumuiya wote,” alisema
Mlinuka.
Alisema kuwa Katibu Mkuu
mpya Liberata Mfumukeko kutoka kutoka Burundi anatakiwa kuendeleza pale
ambapo Dk Sezzibera anapoishia ambapo ni kuhakikisha kwamba unakuwepo
utatu wa ajira katika jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mbali na hilo pia amemtaka
katibu mkuu huyo mpya kuhakikisha protokali ya soko la pamoja kipengele
cha pili cha jumuia ya Afrika Mashariki kinatekelezeka ikiwa ni pamoja
na kuondoa vikwazo vya wananchi kuingiliana kutoka sehemu moja kwenda
nyingine kibiashara pamoja na kutafuta ajira ndani ya nchi wanachama.
Awali Mwenyekiti wa chama
cha waajiri Kenya(FKE) Jacqueline Mugo alisema kuwa nchi wanachama
hazipaswi kuwa na uoga katika yale ambayo yanaonekana kuwa na manufaa na
uhai wa Jumuia ya Afrika Mashariki yakiwemo masuala ya ajira na
mengineyo.
Mkutano wa siku moja
ulikutanisha vyama vyote vya waajiri wa nchi zinazounda jumuia ya Afrika
Mashariki vikiwa na malengo ya kuhakikisha wananchi wa jumuiya hiyo
wanapata ajira popote pale wanapokwenda ndani ya jumuiya ya Afrika
Mashariki.






0 maoni:
Chapisha Maoni