………………………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu,
Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Mfuko wa
Kusaidia Kilimo (PASS) wameingia makubaliano ya kudhamini mikopo kwa
wakulima wasio na dhamana watakaokopa kupitia TADB.
Wakizungumza
katika hafla ya kuwekeana saini makubaliano hayo, yaliyofanyika katika
Ofisi za TADB, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw.
Thomas Samkyi na Mkurugenzi Mkuu wa PASS, Bw. Nicomed Bohay wamesema
kuwa katika kukabiliana na changamoto za ukosefu wa dhamana za uhakika
kunakochagiza ukosefu wa upatikanaji wa mikopo kwa wakulima taasisi hizo
zimekubaliana kuwawekea dhamana wakulima wenye sifa ya kukopesheka
katika Benki hiyo ila wanakosa dhamana waweze kudhaminiwa na PASS.
Bw.
Samkyi amesema pamoja na umuhimu wa Sekta ya Kilimo, bado ukuaji wa
sekta hiyo umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbali mbali kama vile
kiwango kidogo cha uzalishaji; Ufinyu mkubwa wa upatikanaji wa fedha
mikopo kwa ajili ya maendeleo ya kilimo nchini unachangiwa kwa kiasi
kikubwa na mikopo mingi kutoka taasisi za fedha kuelekezwa zaidi kwenye
upande wa biashara za bidhaa; riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo; mikopo
ya muda mfupi; masharti magumu ya kukopa bila kuzingatia hali halisi ya
sekta ya kilimo na mazao ambayo inaathiriwa kwa kiasi kikubwa na
mabadiliko ya hali ya hewa.
“Makubaliano
yetu ya leo, ni ya kihistoria katika kilimo cha nchi yetu kwa kuwa
yataongeza idadi ya wakulima wanaokopesheka kuongezeka na hivyo
kuchangia kufikia malengo ya TADB ambayo ni kusaidia upatikanaji wa
utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania na
kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu
kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza
umaskini nchini,” amesema Bw. Samkyi.
Bw.
Samkyi ameongeza kuwa TADB ikiwa ni Benki Kiongozi katika utoaji wa
mikopo katika sekta ya kilimo ina wajibu wa kuchochea kuinua uzalishaji
wenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa kuendeleza miundombinu muhimu,
mathalani: skimu za umwagiliaji, usafirishaji, hifadhi ya mazao,
usindikaji, na masoko ili kuchagiza kufikia malengo ya Mpango wa Pili wa
Maendeleo unaojielekeza kwenye viwanda.
“Kama
Benki Kiongozi ya maendeleo ya kilimo, pamoja na kuhamasisha mabenki
na taasisi nyingine za kifedha kutoa fedha kwenye mnyororo mzima wa
kilimo, tuna furaha leo kuweza kupata washirika wataowawekea dhamana
wakopaji wetu hivyo kukidhi matakwa ya kisheria kama yalivyowekwa na
Benki Kuu ya Tanzania,” alisema.
Bw.
Samkyi ameongeza kuwa kwa kushirikiana na Serikali, wabia wa kimkakati
na wadau wengine katika kuendeleza sekta ya kilimo, hasa kuboresha na
kutekeleza na juhudi zozote sera zinazohusiana na kuhisha ushiriki wa
wananchi kwenye mifumo ya kifedha. Na pia watatumia fursa hiyo
kuhamasisha upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu na endelevu, ili
kuinua ushiriki wa wakulima wadogo katika mfumo wa kifedha pamoja na
kuhamasisha kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa wakulima wadogo
wadogo.
Kwa
upande wake Bw. Bohay amesema kuwa kwa kuanzia PASS itatoa dhamana
yenye thamani ya shilingi bilioni tatu (3) na zitakuwa zikiongezeka
kadri maombi ya wateja itakavyoongeza.
“Leo
tunafarijika kufikia makubaliano na TADB ambao kimsingi ni wadau wetu
wakuu kwa kuwa sote tumeanzishwa na Serikali pia tuna lengo kuu moja la
kimsingi ambalo ni kuinua ukuaji wa sekta ya kilimo ili kuchagiza ukuaji
wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania,” alisema Bw. Bohay.
Kwa
mujibu wa Bw. Bohay tangu kuanzishwa kwake PASS imeshawekea dhamana
mikopo ya zaidi Bilioni 314 ambayo imewafikia wakulima zaidi ya 323,000
nchini kote.
Kwa upande wa TADB
licha ya uchanga wake imeshakopesa zaidi ya bilioni moja kwa vikundi
nane (8) vyenye jumla ya wakulima wadogo wadogo 857, ambavyo vimetimiza
vigezo mpaka sasa huku ikishughulikia maombi mengine. Ambapo kwa mujibu
wa Bw. Samkyi kabla ya kutoa mikopo hiyo, benki inawatembelea na kutoa
elimu kwa wakulima jinsi ya kuimarisha vikundi vyao, ambapo jumla ya
vikundi 89 vyenye jumla ya wanakikundi 21,526 vimefikiwa mpaka sasa.
TADB
ilianzishwa kwa Sheria Namba 5 ya mwaka 2006 inayosimamia Benki na
Taasisi za Fedha, pamoja na Kanuni za Uanzishaji wa Benki na Taasisi za
Fedha (Development Finance) za mwaka 2012. Lengo la msingi la kuanzishwa
kwa TADB ni kutoa mikopo ya muda mfupi, kati na muda mrefu kwa sekta ya
kilimo ili kuleta mapinduzi ya kilimo nchini.






0 maoni:
Chapisha Maoni