|
WIZARA ya
Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imeziagiza shule zote za binafsi
kuwa na mihula miwili tu ya masomo kwa mwaka badala ya kuwa na mihula
mitatu au minne kama ilivyo kwa sasa katika shule hizo.
Agizo
hilo liko kwenye Waraka wa Elimu Namba Moja wa Mwaka 2015, ambao
unaeleza kuwa kuanzia sasa mihula ya masomo, itakuwa miwili kwa kila
mwaka wa masomo kwa shule zote za serikali na zisizo za Serikali.
Waraka
huo uliosainiwa na Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa
umefafanua kuwa kila muhula, utakuwa na likizo fupi na likizo ya mwisho
wa muhula. Siku za masomo kwa mwaka zitakuwa ni 194.
Waraka
huo pia umeagiza wanafunzi wote, wapumzike mwezi Juni na Desemba na
mashindano ya michezo ya shule za msingi (Umitashumta) na michezo ya
sekondari (Umiseta), ifanyike mwezi Juni wakati wa likizo.
Kutokana
na agizo hilo, wamiliki wa shule zisizo za serikali wametakiwa
kuwasilisha wizara ya elimu kalenda za mihula ya masomo. Nakala ya
waraka huo wamesambaziwa wakaguzi wote wa shule, walioko kwenye kanda na
wilaya kuhakikisha wanazifuatilia shule zote ili ziweze kutii agizo
hilo la Serikali.
Profesa
Bhalusesa alifafanua katika waraka huo, umekazia Waraka wa Serikali
Namba 5 wa mwaka 2012 ambao ulikuwa unaelekeza mihula ya masomo kwa
shule za sekondari na vyuo vya ualimu, ifanane ili kuepusha usumbufu kwa
walimu na kwa wanafunzi.
“Bado
kumekuwa na hali ya kutofautiana kwa tarehe ya kufungua na kufunga shule
katika mihula hiyo kati ya shule za serikali zenyewe na kati ya shule
za serikali na shule zinazomilikiwa na watu binafsi au mashirika ya
dini. Hali hii imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wadau wa elimu wakiwemo
wazazi na walezi wa wanafunzi,” ulisema waraka huo.
Kauli ya Waziri
Akifafanua
kuhusu waraka huo jana, Naibu Waziri Stella Manyanya alisema shule zote
za binafsi na serikali ngazi ya awali, shule ya msingi na sekondari
zitalazimika kufuata maagizo hayo ya Serikali.
Alifafanua
kuwa muhula wa kwanza ulianza Januari 6 hadi 10, 2016 na likizo fupi
ilianza Machi 24, 2016 na kufungua Aprili 4, 2016 na watamaliza muhula
huo Juni 10 hadi 14, 2016. Muhula wa pili ngazi hiyo ya elimu awali
utaanza kati ya Julai 8 na 11, 2016 ambako shule zote zitafunguliwa.
Likizo
fupi wataanza Septemba 8, 2016 na watafungua Septemba 21, 2016 na muhula
wa pili utamalizika kati ya Novemba 30 na Desemba 6, 2016.
Manyanya
alisema kwa upande wa kidato cha tano na sita, muhula wa kwanza utaanza
kati ya Julai 8 hadi 11, 2016 na likizo fupi itaanza Septemba 8, 2016 na
watafungua Septemba 21, mwaka huu wakati likizo ya Desemba watafunga
kati ya Novemba 30 na Desemba 6, mwaka huu.
Naibu
Waziri huyo alisema michezo kwa mashindano ya shuleni itafanyika wakati
wa likizo ya mwezi Machi na ile ya ngazi ya Taifa ifanyike wakati wa
likizo ya mwezi Juni kama ilivyosisitizwa kwenye waraka huo wa elimu.
TAMONGSCO yapinga
Katibu
Mkuu wa Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo binafsi (TAMONGSCO), Benjamin
Nkonya akizungumzia waraka huo, alisema hawakubaliani na agizo hilo la
Serikali la kuwa na mihula miwili mikuu na miwili mifupi kwamba
inawapotezea muda wanafunzi na hivyo kusababisha wafeli kwa wingi kwenye
mitihani yao ya mwisho.
Aliongeza
kuwa mihula ya shule za serikali, jumla yake ni minne na wala sio
miwili. Aliongeza kuwa kwa mtazamo wa haraka, mihula hiyo inamfanya
mwanafunzi akae nyumbani siku nyingi zaidi kuliko mihula mitatu ya shule
zisizokuwa za Serikali.
“Sisi
ambao tuna mihula mitatu mwanafunzi anapoteza wiki sita tu kwa mwaka,
lakini tukiamua kufuata waraka wa serikali mwanafunzi anajikuta
anapoteza wiki nane, hizi ni siku nyingi kwa mwanafunzi kukaa nyumbani,”
alisema Nkonya.
Alisema
Tamongsco baada ya kupokea barua za kuwataka wabadilishe mihula ya
masomo, wameshaiandikia wizara na kuwapa ufafanuzi kuwa licha ya kuwa na
mihula hiyo siku za masomo zimebaki kuwa 194 ambayo inashauriwa na
Serikali yenyewe.
“Sisi
tunagombana na Serikali kwa sababu wanataka tufuate mihula yao, sisi
tunaona kwamba tukifuata hayo maelekezo yao watoto wengi watafeli kama
ilivyo kwa shule za serikali ndio maana tunaendelea kupinga suala hilo,”
alisema Nkonya.
Baadhi ya
shule binafsi zatii Gazeti hili limefanikiwa kupata barua za baadhi ya
wanafunzi wanaosoma shule binafsi zilizoamua kuwaandikia wazazi na
walezi kuwa wako kwenye maandalizi ya kuingia kwenye kalenda ya serikali
ya kuwa mihula miwili ya masomo.
“Serikali
imeagiza shule zote zifuate kalenda kama zinavyofanya shule zake ili
kurahisisha ufuatiliaji wa sera na maagizo mbalimbali ya kielimu. Hivyo
nasi tukiwa ndani ya serikali hii hatuna budi kutii agizo hilo la
Serikali. “Hivyo tunawatangazia kuwa tupo katika hatua za mwisho kuingia
katika utaratibu ambao utatufanya tuwe na mihula miwili huku likizo
ndefu zikiangukia mwezi wa Juni na Desemba,” ilisema barua ya shule moja
binafsi ambayo gazeti hili limepata nakala yake.
Licha ya
shule hiyo, baadhi ya wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule za
msingi za binafsi nao wamekiri kupokea barua kutoka kwa uongozi wa shule
kuwa wanajiandaa kuanda mihula ya serikali, lakini suala la ada
italipwa kwa mihula minne.
“Sisi
katika shule anayosoma mwanangu wameshaanza kuwa na mihula miwili, ila
ada tunalipa mara nne kama ilivyokuwa hapo awali,” alisema mzazi mmoja
ambaye hakutaja jina lake litajwe gazetini.
0 maoni:
Chapisha Maoni