Waziri wa Afya Mhe, Mahmoud
Thabit Kombo kulia akisalimiana na Muakilishi wa Shirika la Afya Duniani
WHO alioko Zanizbar Dk, Ghirmay Andemichael mara baada ya kuwasili
Ofisini kwake Mnazi mmoja Mjini Zanzibar, kupata taarifa ya maradhi ya
kipindupindu yalioanza mwezi Septemba mwaka jana hapa Zanzibar.
Waziri wa Afya Mhe, Mahmoud
Thabit Kombo akizungumza na muakilishi wa Shirika la Afya Duniani WHO
nchini Tanzania Dk, Rufaro Chatora kushoto yake pamoja na ujumbe
aliofuatana nao Ofisini kwake Mnazi mmoja Mjini Zanzibar. Muakilishi
huyo alifika kuangalia hali ya maradhi ya kipindupindu Zanzibar.
Muakilishi wa Shirika la Afya
Duniani WHO Dk, Rufaro Chatora katikati akizungumza na Wakuu wa sekta
mbalimbali katika Wizara ya Afya Zanzibar kuhusiana na Maradhi ya
Kipindupindu Zanzibar. Kushoto yake ni Muakilishi wa WHO aliopo
Zanzibar Dk, Ghirmay Andemichael na kulia yake ni Katibu Mkuu wizara ya
Afya Zanzibar Mohd Saleh Jidawi.
………………………………………………………………………………………………….
NA RAMADHANI ALI/MAELEZO ZANZIBAR
Mwakilishi wa Shirika la Afya
Duniani (WHO) nchini Tanzaia Dkt. Rufaro Chatora amezishauri taasisi za
Serikali, taasisi za kiraia na watu binafsi kila mmoja kutekeleza
wajibu wake katika kukabiliana na maradhi ya kipindupindu nchini.
Amesema maradhi ya kipindupindu
yanapotokea katika nchi moja yanagusa nchi nyingi duniani kutokana na
watu kusafiri kutoka nchi moja kwenda nyengine katika harakati zao za
maisha.
Dkt. Chatora ameeleza hayo
alipokuwa akizungumza katika mkutano na watendaji wakuu wa Wizara ya
Afya na waandishi wa Habari katika ziara yake ya kuangalia hali ya
maradhi ya kipindupindu Zanzibar tokea yalipoanza mwezi Septemba mwaka
jana hadi hivi sasa ambapo watu 2703 wamepata ugonjwa huo.
Amesema maradhi ya kipindupindu
ni rahisi kutibika iwapo kila mtu atatimiza wajibu wake na kufuata
ushauri wa wataalamu wa afya ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia maji
yasiyo salama ambayo ni moja ya chanzo kikubwa cha kupata maradhi hayo.
Mwakilishi huyo wa WHO amesema
Shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Kimataifa
litaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika kukabiliana na maradhi hayo ili kuhakikisha yanamalizika.
Akieleza hali ya kipindupindu
ilivyo hivi sasa Zanzibar katika mkutano huo uliofanyika Wizara ya Afya
Mnazimmoja, Mkurugenzi Kinga na ELimu ya Afya Dkt. Mohd Dahoma amesema
hali bado sio nzuri na wanaendelea kupokea wagonjwa wengi katika kambi
ya Chumbuni.
“Tunapokea wagonjwa kati ya 10
hadi 15 kwa siku katika kambi ya Chumbuni, kwa bahati mbaya jana
tulipokea wagonjwa 20 na kambi moja mpya imefunguliwa katika kisiwa
cha Tumbatu,’’ alisema Dkt. Dahoma.
Amesema jumla ya Kambi 17 za
wagonjwa wa kipindupindu zimefunguliwa katika maeneo mbali mbali ya
Unguja na Pemba na kumi kati yao zimefungwa baada ya kukosa mgonjwa wa
maradhi hayo.
Ameongeza kuwa kati ya wagonjwa
2703 waliogunduliwa na maradhi hayo 34 wamefariki ikiwa ni sawa na
asilimia 1.3 na vijana wenye umri kuanzia miaka 17 ndio walioathirika
zaidi.
Dkt. Dahoma amesema kisiwa cha
Unguja kimekuwa na wagonjwa wengi zaidi wa kipindupindu asilimia 52.3
na Pemba ni asilimia 47.3 huku Mkoa Mjini Magharibi ukiongoza ukifuatiwa
na Mkoa Kaskazini Pemba.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya
amewashauri wananchi kuwawahisha mapema vituo vya afya watu
wanaobainika na dalili za maradhi ya kipindupindu kwa vile imeonekana
wagonjwa wengi wanapopelekwa vituoni afya zao zinakuwa mbaya na matibabu
yanakuwa magumu.






0 maoni:
Chapisha Maoni