![]() | |
|
WAKATI
watuhumiwa wa kesi ya kukutwa na tumbili 61 wakiwa bado rumande kwa
zaidi ya wiki sasa, mke wa mtuhumiwa mmojawapo raia wa Uholanzi, Arten
Vardanian, Mariam, amefariki dunia juzi kwa mshtuko baada ya kusikia
mumewe amekamatwa kwa tuhuma hizo.
Mke huyo
alifariki juzi katika Hospitali ya Staint Grigor Lusavarich Medical
Center katika Jamhuri ya Armenia akiwa katika chumba cha uangalizi
maalumu (ICU). Taarifa ya kifo iliyotolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa
Huduma ya Dharura katika hospitali hiyo, Gagik Manukyan, ambayo nakala
yake gazeti hili linayo, ilithibitisha kifo hicho na sababu kuwa
mshtuko.
Hata
hivyo ilieleza kuwa Mariam alifikishwa hospitalini hapo akiwa na hali
mbaya na ilizidi, baada ya mshtuko wa taarifa kuhusu mumewe na alifariki
juzi Machi 30, mwaka huu saa 8:45 alasiri majira ya Armenia.
Taarifa
hiyo ilisema Mariam alifikishwa hospitalini hapo Machi 9, mwaka huu,
akiwa katika hali isiyo nzuri akiumwa ugonjwa ambao hawakuubainisha na
ilieleza kuwa juzi baada ya kusikia kukamatwa kwa mumewe akituhumiwa
kusafirisha tumbili, alipata mshtuko na kufa.
Wakili
anayewatetea watuhumiwa hao wa Kampuni ya Stratton and Company Advocates
ya jijini Arusha, Kisaka Mzava, alithibitisha pia suala hilo. Wakili
Mzava aliwataja watuhumiwa anaowatetea kuwa ni Arten Vardanian (53),
raia wa Uholanzi na Edward Vardanian (44), raia wa Russia na kwamba ni
ndugu.
Watuhumiwa
hao pamoja na wengine akiwemo Ofisa Mfawidhi Kanda ya Kaskazini
anayehusika na matumizi endelevu ya wanyamapori nchini, (CITES),
Nyangabo Musika, Idd Misanya anayetuhumiwa kuuza wanyama hao na
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dk
Charles Mulokozi na Mkurugenzi wa Manyara Bird, Juma Eliasa nao
wanashikiliwa.
Tangu
kukamatwa kwa watuhumiwa hao Machi 24, mwaka huu saa 1 usiku Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kuchukuliwa maelezo siku
tatu baadaye katika kituo cha Polisi uwanjani hapo, watuhumiwa hao bado
hawajafikishwa mahakamani mpaka jana.
Wakili
anayewatetea, alisema tumbili wanaodaiwa kukamatwa, sio wa wateja wake,
isipokuwa ni wa mfanyabiashara mmoja, Artur Khatcharyan, raia wa Armeria
anayemili kampuni ya Zoo Fauna Art. LLC ya nchini humo. Idadi ya watu
waliokamatwa hadi jana kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa, ni saba.







0 maoni:
Chapisha Maoni