RAIS John
Magufuli amesali Ibada ya Jumapili kijijini kwao wilayani Chato kwa
mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais, na kusisitiza Watanzania wote
kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani na kuwataka
kupendana, kushirikiana na kutobaguana.
Dk
Magufuli ambaye yuko mapumzikoni nyumbani kwake Lubambangwe katika
kijijini cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita, aliungana na waumini
wenzake wa Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato, kusali ibada ya
Jumapili ya Pili ya Pasaka. Pamoja na mambo mengine, aliwausia
Watanzania wote kuendelea kuliombea Taifa ili liendelee kuwa na amani.
“Niwaombe
Watanzania wote tuendelee kushirikiana na kushikamana, kwa umoja wetu
na siku zote tumtangulize Mungu mbele. Wakati tunaadhimisha wiki moja
baada ya kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Yesu Kristo alikufa kwa
sababu ya dhambi zetu, sisi wote tujitahidi kufuata matendo ya Yesu
Kristo ya kusameheana, kupendana, kushirikiana na tusibaguane,”
alibainisha Rais Magufuli.
Pamoja na
Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth, ibada hiyo ilihudhuriwa na Waziri
Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga na mkewe Mama Ida Odinga, ambao ni
familia rafiki ya Rais Magufuli waliowasili Chato juzi jioni kwa
mapumziko wakitokea Nairobi, Kenya.
Katika
salamu zake kwa waumini wa Parokia ya Chato, Odinga aliwashukuru
Watanzania kwa uhusiano mzuri walionao na Wakenya, huku akitoa mfano wa
jinsi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyojitoa
kupigania uhuru wa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Kenya.
Odinga
alitoa mfano wake mwenyewe kuwa Mwalimu Nyerere alimpatia pasi ya
kusafiria ya Tanzania aliyoitumia kwa miaka mitatu akienda kusoma nje ya
nchi baada ya utawala wa Kikoloni wa Kenya kukataa kumpa pasi hiyo.
Kuhusu
urafiki wake na Rais Magufuli, Odinga alisema, “urafiki huo ulianza
tangu Rais Magufuli alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na yeye kuwa
Waziri mwenye dhamana ya ujenzi wa Kenya, ambapo mara kadhaa
walibadilishana uzoefu na kushirikiana katika mipango ya miradi ya
ujenzi wa barabara, na kwa umuhimu huo ametoa mwito kwa nchi za Jumuiya
ya Afrika Mashariki kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliojengwa na
waasisi wake wakiongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.”
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amlitoa mchango wa Sh milioni 10 kwa
Kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato mkoani Geita kwa ajili ya
kuchangia upanuzi wa kanisa hilo. Fedha hizo zilikabidhiwa na Kaimu
Mnikulu Ngusa Samike katika misa ya pili ya ibada ya Jumapili ya Pili ya
Pasaka iliyofanyika kanisani hapo jana.
Kabla ya
misa hiyo ya pili, Rais Magufuli na mkewe Mama Janeth wakiwa pamoja na
Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga na mkewe Mama Ida, walisali
misa ya kwanza, na Rais Magufuli aliahidi kuchangia Sh milioni 10 kwa
ajili ya upanuzi wa kanisa hilo ambao unaendelea.
Katika
misa hiyo, Paroko wa Parokia ya Chato, Padri Henry Mulinganisa alieleza
kuwa kanisa hilo linatarajia kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake
baadaye mwaka huu, na kwamba maadhimisho hayo yanakwenda sambamba na
upanuzi wa kanisa ambao unachangiwa na waumini wenyewe.
Padri
Mulinganisa alimshukuru Rais Magufuli kwa mchango huo, na amemuahidi
kuwa utatumika vizuri ili uendeleze upanuzi wa kanisa hilo pamoja na
michango ya waumini wengine.







0 maoni:
Chapisha Maoni