CHAMA cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimewataka viongozi wa serikali na chama kuharakisha kutoa
misaada kwa waathirika wa mafuriko bila ya kujali tofauti zao za
kisiasa.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akitembelea
maeneo mbali mbali ya Zanzibar yaliyoathiriwa na mafuriko hayo.
Alisema mamia ya watu waliopata
mafuriko hayo kwa sasa wanahitaji msaada wa haraka ili waweze kupata
mahitaji ya msingi kama walivyo watu wengine.
“CCM itaendelea kuungana na
wananchi waliopata athari ya mafuriko kwa kutoa misaada ya hali na mali
kwa lengo la kuhakikisha wanapita salama katika kipindi hiki kigumu cha
mvua za masika zinaendelea nchini”., alisema Vuai.
Akifafanua zaidi Vuai alisema CCM
inakuwa na misimamo ya kisiasa wakati wa upigaji wa kura pekee lakini
sio kwenye masuala ya majanga na matatizo ya kitaifa kwani inaamini kuwa
majanga hayo yanawakumba wananchi wote bila ya kujali tofauti zao za
kisiasa.
“Misimamo ya chama chetu
inajitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi wa kisiasa lakini wakati wa
majanga na matatizo ya kitaifa kamna haya tunabaki kuwa wamoja katika
kuwasaidia na kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali tofauti zetu za
kisiasa.
Kwa niaba ya chama chetu natoa
pole na kuwasihi wananchi wote waliokumbwa na mafuriko kuendelea kuwa
wavumilivu kwa kipindi hiki na tunawaahidi kuwa chama na serikali
tutaendelea kuwasaidia wahanga wa mafuriko hayo kadri ya uwezo
utakavyoruhusu.”, alifafanua Vuai.
Aliwashauri baadhi ya wananchi
waliojenga katika maeneo ya mabonde na sehemu za mitaro ya maji ya mvua
kuhama kwa haraka katika maeneo hayo kabla hawajapata athari za
kuharibikiwa na makaazi yao.
Pamoja na hayo, Vuai alifafanua
kuwa CCM itaendelea kuzishauri taasisi za serikali zinazohusika na
masuala ya makaazi na miundo mbinu ya barabara kutafuta njia mbadala za
kiutaalamu zitakazosaidia kumaliza tatizo la maji ya mvua kujaa katika
baadhi ya mitaa ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa takwimu
zilizopatikana katika ziara hiyo zinaeleza kuwa takriban nyumba 720
zimekubwa na mafuriko kati ya hizo 196 wamehama kabisa makaazi yao baada
ya nyumba zao kuharibiwa kabiwa kabisa na mafuriko hayo.
Katika ziara hiyo yenye madhumuni
ya kuwapa pole na kutathimini athari ya mafuriko hayo, Naibu Katibu
Mkuu Vuai Ali Vuai, aliungana na viongozi mbali mbali wa chama na
Serikali wakiwemo Wabunge, Wawakilishi, Madiwani na Masheha wa maeneo
husika.
Naibu Katibu Mkuu Vuai,
alitembelea maeneo 11 yaliyopata majanga hayo yakiwemo Timba, Karakana,
Chumbuni, Kihinani, Bububu, Kikwajuni, Kisimajongoo, Kwahani,
Matarumbeta, Sebreni, Jang’mbe ya Migombani na Mfenesini.
0 maoni:
Chapisha Maoni