Postedy by Esta Malibiche on August 3.2016
Na Raymond Mushumbusi WHUSM
Zikiwa zimebaki siku chache kabla kuanza rasmi michezo ya 31 ya Olimpiki mjini Rio de Janeiro nchini Brazilinayotarajiwa kuanza Ijumaa ya Agosti 4, 2016 katika mji wa Sao Paulo na Rio De Jeneiro nchini Brazil,
wawakilishi
wa Tanzania katika michuano hiyo wamepata baraka zote kutoka kwa
Serikali na kukabidhiwa bendera ya Taifa kabla ya kwenda kuipeperusha
nchini Brazil.
Akikabidhi
bendera kwa timu hiyo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Mhe. Annastazia Wambura aliwataka washiriki wanaokwenda
kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Olimpiki mwaka huu huko Rio De
Jeneiro nchini Brazil kujituma na kuhakikisha wanafanya vizuri ili
warudi na medali.
Mhe.
Annastazia Wambura alisema kuwa wanapokwenda kuiwakilisha waamini kuwa
macho na masikio ya watanzania wote yapo kwao kwahiyo wajitahidi kadri
ya uwezo wao kuweza kuhakikisha watakapokuwa wanarejea basi waje wakiwa
wamevaa medali zao.
" Mnakwenda
katika mashindano ya Olimpiki macho yote ya watanzania yapo kwenu
tunategemea mkiwa mnarudi basi tutakuja kuwapokea mkiwa na medali zenu
kifuani na hilo linawezekana kama mtajituma mkiwa na ari ya ushindi".
Aidha Katibu
Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania , Filbert Bayi alisema kuwa kwa
mwaka huu washiriki wamekaa kambi katika sehemu tofauti nchini na
wengine wakiwa nje ya nchi na hilo limefanikisha kuweza kujifua vyema na
kujiandaa ili kuweza kurejesha ushindi nyumbani.
Akizungumzia
mara baada ya kukabidhiwa bendera Kocha wa timu ya kuogelea Bw.
Alexandra Mwaipasi alisema kuwa wachezaji wake wameiva kwani mwanzoni
walikuwa na changamoto ya kupata mabwawa yenye viwango vinavyoendana na
mashindano hayo ili kwa matayarisho aliyowapatia wachezaji wake
anahakika watarudi na medali.
Moja ya
washiriki wa mchezo wa kuogelea katika mashindano ya Olimpiki kwa mwaka
2016 Magdalena Mosha alisema kuwa amejiandaa vizuri na anaamini kwa
miaka aliyoshiriki kwenye mashindano ya Olimpiki ya Beijing na London
yamempa uelewa zaidi wa nini anatakiwa kufanya na kuyafanyia kazi
mazoezi aliyoyapata nchini Australia ili kurudi na ushindi.
Naye mmoja wa
wawakilishi katika mchezo wa Judo, Adrew Thomas alisema amejiandaa
vizuri kwa ajili ya mashindano hayo na yuko tayari kuiwakilisha Tanzania
na kuleta ushindi na pia kuitangaza Tanzania katika michezo na utalii
uliopo kwa kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini.
Kwa upande
wake Sara Ramadhani ambaye ni mwakilishi mwanamke pekee katika mshindano
hayo kwa wakimbiaji wa Marathon alisema yuko vizuri kuipeperusha
bendera ya taifa na kuitangaza Tanzania kimataifa kwa kushindana na
kushinda medali hivyo kuiletea sifa nchini.
Mmoja wa
wadhamini wa safari hiyo kampuni ya Multichoice Africa, imewataka
washiriki hao kujituma zaidi kwani watanzania wote watakuwa
wanawaangalia kupitia chaneli zao zinazopatikana kwenye kisimbuzi cha
DSTV.
Katika
mchango wao kwa wawakilishi hao Kampuni ya visimbuzi ya Dstv imetoa
mchango wa kuwakutanisha pamoja kwa kuandaa hafla ya kuwaaga wawakilishi
hao ikiwa ni moja ya kuwatia moyo waende kupambana na kushinda katika
michezo mbalimbali na kuliletea sifa taifa.
Akizungumza
kwa niaba ya kampuni hiyo Mkurugenzi wa Multichoice Tanzania Maharage
Chande alisema mwaka huu mashindano yote yatakuwa yakioneshwa moja kwa
moja kupitia channeli za Super Sport na itawapa fursa watanzania
kuwashuhudia wawakilishi wao kwenye mashindano hayo makubwa duniani.
Bodi ya
Utalii nayo haikuwa nyuma kuwapa nguvu na morali wawakilishi wa Tanzania
katika mashindano ya Olimpiki kwenda kufanya vizuri katika mashindano
hayo na pia kutangaza vivutio vilivyopo nchini kwa mataifa mbalimbali
yanayoshiriki mashindano hayo kwa kuwapatia vifurushi kwa ajili ya
kusambaza ujumbe kuhusu utalii wa Tanzania.
Akitoa nasaha
zake kwa wawakilishi hao Mkurugenzi wa Utalii Bw. Godfrey Tengeneza
aliwaasa wawakilishi hao kujituma kwa bidii na kutangaza nchi kupitia
michezo na pia watumie fursa hiyo kutangaza vivutio vilivyopo Tanzania
kwa kueneza habari kuhusu utalii Tanzania.
“Mtakapokuwa
huko mbali na kushiriki katika michezo muitangaze nchi yetu kwa vivutio
vilivyopo nchini ili tuzidi kupata watalii wengi kutoka duniani kote”.
Timu ya
Tanzania inayoenda kushiriki mashindano ya 31 ya Olimpiki nchini
Brazil inawakilishwa na wachezaji saba ambao ni waogeleaji wawili
Magdalena Mosha anayeenda kwa mara ya tatu kwa upande wa wanawake huku
Hilal Hilal akienda kwa mara ya kwanza kwa upande wa wanaume na wote
watakuwa ni waogeleaji kwa umbali wa mita 50.
Wengine ni
Fabian Joseph, Said Juma Makula na Alphonce Felix Simbu watakaokimbia
marathon kwa wanaume na Sara Ramadhani ambaye ni mwanamke pekee
anayeiwakilisha Tanzania katika mbio za marathon.
Na kwa upande wa mchezo wa Judo Tanzania itawakilishwa na Adrew Thomas Mulugu katika uzito wa kilogramu 73.
Katika mashindano ya Olimpiki mwaka huu takribani M yanatarajiwa
kushindana katika michezo mbalimbali huku Marekani ikiongoza kuwa na
wachezaji wengi zaidi katika mashindano hayo ikiwa na wachezaji 550
ikifuatiwa na Brazil iliyo na wachezaji 450 na China inayowakilishwa na
wachezaji 380.
0 maoni:
Chapisha Maoni