Jumatano, 3 Agosti 2016

Wananchi Zanzibar watakiwa kulipia huduma ya maji

tankNa Rahma Khamis Maelezo -Zanzibar
Wananchi wa Zanzibar wametakiwa kulipia huduma ya maji kwa wakati ili kuweza kupata huduma hiyo kwa ufanisi zaidi na kuepukana na usumbufu unaoweza kujitokeza.
Wito huo umetolewa na Afisa Uhusiano wa  Mamlaka ya Maji Zanzibar  (ZAWA) Zahour Suleiman  Ofisini kwake  Msikiti Mabuluu Mjini Zanzibar wakati akitoa maelezo kuhusiana na ulipaji wa huduma ya maji.
Amesema maji ni moja ya huduma muhimu katika maisha ya wananchi  hivyo ni muhimu  kuhakikisha yanapatikana muda wote  na suala la  kulipia huduma hiyo ili iwe endelevu  ni jambo la msingi.
Afisa huyo amefahamisha kuwa badhi ya wananchi wamekuwa na  mwamko mdogo katika kulipia huduma ya maji na  kusababisha  Mamlaka kukosa uwezo wa kutoa huduma hiyo kwa ufanisi.
Aidha amesema kuwa kwa sasa huduma hiyo inaelekea kuzidiwa kutokana na kukuwa kwa harakati za kimaendeleo hasa kwa matumizi ya kilimo ambacho kinatumia maji mengi  ukilinganisha na matumizi ya majumbani.
Afisa huyo amefahamisha kuwa wameanzisha  utaratibu  wa kupita katika maeneo kwa lengo la kutoa elimu kuhusiana na  umuhimu wa kulipia maji na  wale watakaoshindwa kuufahamu mpango huo Mamlaka huwapa onyo na baadae kusitishwa kupata huduma.
Sambamba na hayo Zahour amewashauri wanajamii kufuata sheria bila ya kushurutishwa kwa kulipia maji kwa wakati ili kuipa uwezo Mmlaka ya maji kutekeleza wajibu wake wa kuwapatia  wananchi huduma hiyo kama kawaida.

0 maoni:

Chapisha Maoni