Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi akimuonesha athari za mvua Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia kwake) wakati akikagua daraja la Koga lililoathirika. Daraja hilo linaunganisha mkoa wa Katavi na Tabora.
……………………………………………………………………………………………
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali ipo katika hatua za
mwisho kuanza mradi wa ujenzi wa barabara ya Tabora-Koga-Mpanda yenye
urefu wa Km. 356 kwa kiwango cha lami ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya
Rais wa Awamu ya Tano aliyoitoa kwa wananchi wa Mikoa ya Katavi na
Tabora.
Ametoa kauli hiyo wilayani Sikonge
mkoani Tabora, mara baada ya kukagua barabara hiyo ambapo pamoja na
mambo mengine amesema ujenzi huo unatarajia kuanza rasmi hivi karibuni.
‘Ujenzi wa barabara hii tumeugawa
katika sehemu tatu ili kuharakisha utekelezaji wake, tutahakikisha
ifikapo mwisho wa mwaka huu, makandarasi wote watatu watakuwa katika
maeneo yao ya kazi’, amesema Prof. Mbarawa.
Amesisitiza kuwa wananchi
wanaostahili kulipwa fidia watalipwa kwa wakati kwa kuwa takribani
shilingi bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Prof. Mbarawa pia amekagua daraja
la Koga linalounganisha Mkoa wa Katavi na Tabora na kuwataka viongozi wa
mikoa hiyo kuhakikisha kuwa magari yasiyozidi tani tatu ndio yanayopita
katika daraja hilo ili kuepusha ajali hadi ukarabati mkubwa
utakapofanyika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mlele,
Kanali Mstaafu Issa Nziku amemuomba Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano kupandisha hadhi baadhi ya barabara katika Wilaya hiyo ili
zihudumiwe na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutokana na uwezo
mdogo wa Halmashauri hiyo kuzikarabati kila wakati.
Katika Hatua nyingine Prof.
Mbarawa amekagua uwanja wa Ndege wa Tabora na kuwataka viongozi wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga
Tanzania(TCAA) kuangalia namna bora ya ukarabati wa kiwanja hicho ili
uruhusu ndege kubwa kutua na kuongeza biashara.
Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya
siku saba ya kukagua miundombinu ya taasisi zilizo chini ya Wizara yake
katika mikoa ya Magharibi ili kuifungua kanda hiyo kimiundombinu na
hivyo kufufua fursa za kiuchumi.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano






0 maoni:
Chapisha Maoni