Mkurugenzi wa Kampuni ya
Advanced Security Limited, Juma Ndambile ambaye pia ni meneja wa bondia
Francis Cheka akimwaga sera baada ya kupitishwa kuwania nafasi ya
Ukatibu Mkuu kwa Chama Cha Soka cha Manispaa ya Kinondoni (KifA)
Mkurugenzi wa Kampuni ya
Advanced Security Limited, Juma Ndambile (wa kwanza kushoto) akiwa na
bondia wake Francis Cheka wakati wa kukabidhi mkanda wa ubingwa Super
Middle kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye
(wa kwanza kulia).
………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu
Meneja wa bondia Francis Cheka, Juma
“Chief” Ndambile amesema kuwa ameamua kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa
Chama Cha Soka Cha Kinondoni (KIFA) kwa lengo la kuendeleza mchezo huu
katika manispaa hiyo.
Uchaguzi Mkuu wa Kifa umepangwa
kufanyika Mei Mosi na utawashirikisha jumla ya wagombea 33
waliopitishwa na kamati ya Uchaguzi ya chama hicho.
Ndambile ambaye ni Mkurugenzi
wa kampuni maarufu ya ulinzi yaAdvanced Security Co. Limited alisema
kuwa kabla ya kuamua kuwania nafasi hiyo, alifanya uchunguzi wa kina na
kugundua kuwa pamoja na Kinondoni kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji,
tatizo kubwa ni uongozi.
Ndambile alisema kuwa Kinondoni
ina wadau wengi wa mpira wa miguu, lakini cha kushangaza mpaka sasa
hakuna timu inayoshiriki LigiKuu ya Tanzania Bara na kubaki na timu za
daraja la kwanza, pili na madaraja mengine ya chini.
Alisema kuwa Kinondoni ina timu
nyingi sana za mpira wa miguu ambazo zinaibua vipaji kutoka chini na
wengine kuwa wachezaji wa kutegemewa wa timu za Ligi Kuu na timu ya
Taifa, lakini kutokana na mfumo wa uongozi kuwa si mzuri, wachezaji hawa
wanahamia timu nyingine na kuzipandisha daraja kucheza ligi kuu na
Kinondoni kubakia nyuma.
“Kungekuwa na uongozi bora
ambao ungekuwa unafuatilia kikamilifu wachezaji na klabu, leo
tusungekuwa na timu mbili tu daraja la kwanza, Friends Rangers na KMC
zingekuwa ligi kuu na nyingi zingekuwa daraja la kwanza, sisi tumekuwa
mishumaa wa kutoa mwanga huku tukiteketea,”
“Siri kubwa ya kuondokana na
hili ni kutafuta wadhamini kwa timu zetu na kuboresha hali ya wachezaji,
Kinondoni ni Manispaa tajiri Tanzania kwa kutumia wadhamini,
waachezaji wangepata vipato vizuri na kupunguza kazi kwa viongozi
kuhangaika huku na kule kusaka fedha za uendeshaji wa timu,” alisema
Ndambile.
Alifafanua kuwa mbali ya
maslahi ya waamuzi, pia atahakikisha kunakuwa na uhusiano mzuri na vyama
vishirikishi katika soka kama madaktari wa michezo, makocha, soka la
vijana, soka la wanawake, Suptanza na wadau wengine ili kujenga umoja
wenye nguvu.
Alisema kuwa yeye yupo tayari
kufanya kazi wadau wote wa mpira wa miguu pamoja na kuhimarisha zaidi
uhusiano wa serikali ya Manispaa ya Kinondoni na chama kwani ndiyo
nyenzo pekee ya kufikia hatua kubwa kabisa ya maendeleo.
“Sitakuwa kiongozi wa kukaa
ofisini, kama mtendaji nitakuwa mfuatiliaji wa kila jambo kama ilivyo
kwa viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli,
tunahitaji kufanya kazi na si kutafuta sifa,” alisema.
Mbali ya Ndambile, wagombea
wengine katika nafasi hiyo ni Hashim Abdallah, Selemani Sufiani,
Ramadhani Kampira, Funua Ally, Isack Mazwile na Raymond Solomon.
0 maoni:
Chapisha Maoni