WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa
Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kufuatilia maendeleo ya mradi wa
umwagiliaji wa Narunyu katika kata ya Kiwalala wilayani Lindi.
Hatua hiyo imekuja baada ya
wananchi wa kata hiyo kusimamisha msafara wa Waziri Mkuu, Majaliwa
katika eneo la Kiwalala jana na kumuomba awasaidie kuhusu hatma ya mradi
wao wa umwagiliaji ambao walitakiwa wakabidhiwe tangu mwaka 2014.
Awali muwakilishi wa wananchi
hao, Mohammed Bakar alisema kuwa mradi huo uliogarimu shilingi milioni
600 ulitakiwa uwe tayari umekabidhiwa kwa wananchi, lakini hadi sasa
bado na hata banio halijakamilika, hivyo wanashindwa kuendelea na kilimo
katika eneo hilo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu mradi huu
bado haujaanza ila tulishangaa wakati wa mbio za mwenge mwaka 2014
ilisomwa taarifa kwamba wakazi wa Kiwalala wananufaika na mradi wa
kilimo cha umwagiliaji wa Narunyu jambo ambalo si kweli kwani mradi huu
haujawahi kufanya kazi na hata banio hakuna,” amesema.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema
malalamiko hayo ya wananchi wa Kiwalala lazima yafanyiwe kazi, hivyo
amemuagiza mkuu wa mkoa wa Lindi, Zambi kuhakikisha anakwenda kwenye
kata hiyo kulipatia ufumbuzi suala hilo.
“Kweli kuna miradi ambayo
inaelekezwa na watu kwa viongozi kuwa imekamilika wakati bado, namuagiza
mkuu wa mkoa kulifanyia kazi jambo hili,” amesema.
Pia amesisitiza kwamba serikali
hii si ya kuleana, mtu atakayebainika kukwamisha miradi ya maendeleo
watamalizana naye hapo hapo, hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira
kwani taarifa yao imepokelewa na inafanyiwa kazi.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa huo,
Zambi amesema tayari ameshapata taarifa za tatizo la mradi huo na
kwamba atafanya ziara kwenye eneo hilo na mtu atakayebainika kutafuna
fedha za mradi huo atamuwajibisha hapo hapo kwa sababu yeye hataki
kutumbuliwa.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu
0 maoni:
Chapisha Maoni