Na Elias Malima , NEC
…………………………………
Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba
na Utawala imeipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kufanikisha
kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Rais Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 vizuri
na kuiacha nchi ikiwa na Amani, utulivu na Usalama.
Hayo yalisemwa jijini Dar ess
Salaam jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh Najma Murtaza Giga
walipokutana na Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika Ukumbi
wa Mwalimu Nyerere convention Center katika kikao mahsusi cha Kupitia
Bajeti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Aidha, pongezi hizo kwa NEC
zilitolewa na wajumbe wa pande zote mbili yaani wa Chama tawala na wale
wa upinzani wa kamati hiyo kwa nyakati tofauti. Baadhi ya wabunge hao ni
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mheshimiwa Najma Murtaza Giga(CCM),
Twahir Awesu Mohammed (CUF) na Nassor Suleiman Omar (CUF).
Alisema ni jambo la heri sana
pale ambapo taasisi ama mtu anafanya kazi ya kutukuka kupewa sifa yake
na kupewa moyo ili aendelee na moyo wa kufanya kazi kwa bidii na
hatimaye kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi si tu kwa manufaa ya
taasisi yake bali hata kwa Taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Uchaguzi Kailima Ramadhan aliiambia kamati hiyo kwamba haikuwa kazi
rahisi kuendesha na kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na Nchi
ikaendelea kuwa na amani na utulivu kwani ushindani wa kisiasa ulikuwa
mkubwa kiasi cha kutishia maisha ya watanzania.
“Tulijitahidi kwa kadiri ya uwezo
wetu kufuata Sheria Kanuni na taratibu za kusimamia Uchaguzi pamoja na
kwamba Bajeti ilikua haitoshi hasa wakati tunaanza zoezi la Uandikishaji
wa Wapiga Kura kwa kutumia Teknolojia ya BVR ambapo tulilazimika
kuandikisha wapiga Kura kwa kuhamahama” Alisema Kailima.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya
waziri Mkuu Sera Uratibu na Bunge Jenista Mhagama aliwashukuru wabunge
kwa niaba ya Serikali kwa jinsi walivyothamini na kutambua Kazi kubwa
iliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuahidi kufikisha Serikalini
mawazo ya kuitafutia Tume fedha kwaajili ya Tume kuzipatia Asasi za
Kiraia zinazotoa Elimu ya Mpiga Kura kwani lilijitokeza suala la Ukosefu
wa Fedha za Kuendeshea Elimu hiyo.
Bajeti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 ni jumla ya Tsh 4,830,537.167/= ikiwa ni fedha za matumizi ya kawaida OC Miradi ya Maendeleo pamoja na Mishahara ya watumishi.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015
ulifanyika tarehe 25 Oktoba ambapo aliyekua Mgombea Urais kwa tiketi ya
Chama cha Mapinduzi CCM Mh.Dkt John Pombe Magufuli aliibuka Mshindi.
0 maoni:
Chapisha Maoni