……………………………………………
Wizara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi
imekanusha kodi ya ng’ombe iliyoripotiwa na Umoja wa wafanyabiashara wa
Mifugo na Mazao yake wa Wilaya ya Kinondoni.
Taarifa hii imetolewa na Katibu
Mkuu (Mifugo) wa Wizara hiyo Dkt. Mary Mashingo baada ya kuyaona
malalamiko ya wafanyabiashara hao kwenye baadhi ya vyombo vya habari
nchini.
Katika taarifa hiyo wizara
imekanusha kuwa kodi ya ng’ombe siyo shilingi 18,500 kama ilivyoripotiwa
na wafanyabiashara hao bali ni shilingi 12,000 ambayo inatambulika
kisheria.
“Wizara yetu inapenda kutoa
ufafanuzi juu ya kodi inayotozwa katika machinjio ya Kimara kama
ifuatavyo: ushuru wa soko shilingi 5000, ushuru wa kusafirisha mifugo
shilingi 1500, ushuru wa ukaguzi wa wanyama shilingi 2500 pamoja na
gharama za machinjio shilingi 3000 kwa kila kichwa cha ng’ombe ambapo
jumla yake ni shilingi 12,000”alisema Dkt.Mashingo.
Aidha,taarifa hiyo imeelezea
kuhusu kupitisha ng’ombe katika soko la upili la Pugu kabla ya
kuwapeleka katika machinjio ya Kimara kuwa ni kwa ajili ya kuwafanyia
vipimo vya afya ng’ombe hao kabla ya kuchinjwa pamoja na kulipia tozo ya
Serikali.
Taarifa hiyo pia imefafanua baadhi
ya sababu za kufungwa kwa machinjio ya Kimara tangu Aprili 9 mwaka huu
zikiwemo za baadhi ya wafanyabiashara kupeleka ng’ombe katika machinjio
hayo moja kwa moja bila kupitia Pugu ambalo ni kosa kisheria pamoja na
uchafu uliokithiri katika machinjio hayo.
Katika kufanya juhudi za kupambana
na matatizo haya,Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inajipanga kukutana
na wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake ili kuwaelimisha zaidi
kuhusu Sheria, Kanuni, na Taratibu zinazopaswa kufuatwa katika ufanyaji
wa biashara hii.






0 maoni:
Chapisha Maoni