Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa
kodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo
akionesha kwa waandishi wa Habari leo Jijini Dar es salaam moja ya CD
zilizokamatwa wakati wa msako wa kubaini wale wote wanaojihusisha na
uuzaji na usambazaji wa kazi za wasanii bila kuwa na stempu za kodi
katika bidhaa za filamu na muziki. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya
Filamu Bi Joyce Fissoo na mwisho kulia ni Afisa Habari wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania Bi Mariam Mwayera.
Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipa
kodi toka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo
(katikati) akitoa wito leo Jijini Dar es salaam kwa wasambazaji na
wauzaji wa kazi za Filamu na muziki kuzingatia sheria na Kanuni
zinazosimamia sekta hiyo kwa kuwa Serikali itawachukulia hatua kali wale
wote watakaoenda kinyume cha sheria na taratibu zilizopo ikiwemo
kutozwa faini isiyopungua milioni tano au kifungo kisichopungua miaka
mitatu jela. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi Joyce
Fissoo,Kushoto ni Afisa Utamaduni wa Bodi ya filamu Bw. Wilhadi Tairo.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu
Bi Joyce Fissoo akifafanua kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam kuhusu mikakati ya Bodi hiyo kuhakiksha kuwa kazi za wasanii wa
filamu zinaendana na maadili ya Taifa.kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma na
Elimu kwa Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. Richard Kayombo.
Baadhi ya waandishi wa Habari
wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya
Filamu Tanzania ukilenga kueleza Mikakati ya Serikali katika kulinda
haki za wasanii wa filamu na Muziki zinalindwa.
( Picha na Frank Mvungi- Maelezo)
……………………………………………………………………………………………………………..
Na Fatma Salum (MAELEZO)
Serikali kupitia Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) imeahidi kuendeleza msako wa wafanyabiashara wote
wanaouza kazi za filamu na muziki bila kubandikwa stempu halali za kodi
ili kuzilinda kazi hizo kwa ajili ya kuwanufaisha wasanii na kuhakikisha
Serikali inapata mapato yake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Huduma kwa Mlipa Kodi kutoka TRA Richard Kayombo wakati akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.
Kayombo amesema TRA kwa
kushirikiana na wadau wa tasnia ya muziki na filamu imedhamiria
kuhakikisha kuwa bidhaa za filamu na muziki zenye stempu za kodi ndizo
zinazoingizwa sokoni ili kulinda kazi za wasanii wa taifa letu dhidi ya
dhuluma zinazofanywa na baadhi ya wafanyabiashara.
“Msako huu endelevu utahusisha
kukamata bidhaa zote ambazo hazijabandikwa stempu za kodi na
kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa sheria.” Alieleza Kayombo.
Aidha Kayombo amefafanua kuwa kwa
kipindi cha mwezi Februari na Machi 2016, TRA kwa kushirikiana na
Dalali wa Mahakama Yono Auction Mart & Company Limited ilifanya
msako jijini Dar es Salaam na kukamata jumla ya CD na DVD zenye thamani
zaidi ya shilingi Bilioni 1.3 ambazo zilisambazwa bila kufuata sheria
hivyo kukwepa kodi ya ushuru ipatayo shilingi Milioni 31.9 na gharama za
stempu zaidi ya shilingi Milioni 11.1.
TRA inawatahadharisha wale wote
wanaosambaza na kuuza kazi za filamu na muziki ambazo hazijabandikwa
stempu kuacha mara moja na kufuata utaratibu wa kupata stempu hizo
katika ofisi za TRA ili wawe na uhalali wa kuuza bidhaa hizo kinyume
chake hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
0 maoni:
Chapisha Maoni