Waziri Mkuu, Kassim Majliwa
akiteta na wapiga kura kijijini kwake Namdagala wilayani Ruangwa
Aprili 11, 2016., Alikuwa katika ziara ya siku tatu jimboni Ruangwa.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………………………………………..
WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa amesema vijiji 42 vya
wilaya ya Ruangwa vitaunganishiwa umeme katika Mradi wa Usambazaji Umeme
Vijijini (REA) awamu ya tatu.
Amesema hadi sasa tayari vijiji
48 vya wilaya hiyo vimeunganishiwa umeme na kwamba lengo lake ni
kuhakikisha vijiji vyote 90 vinapata huduma hiyo, hivyo amewaomba
wananchi kuendelea kuwa na subira.
Waziri Mkuu, Majaliwa ameyasema
hayo jana alipokuwa akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa
vijiji vya Michenga, Chinongwe, Makanjiro na Chinokole katika mikutano
ya hadhara aliyoifanya wilayani Ruangwa.
“Niliwaahidi kuwatumikia,
kuwahudumia na kuwasemea ndani na nje ya nchi, nawahakikishia kuwa
sitowaangusha hivyo endeleeni kuwa na subira, nitafanya mambo mengi ya
maendeleo kama isemavyo kauli mbiu yangu, Ruangwa kwa maendeleo
inawezekana.” amesema.
Kwa upande wake Meneja wa TANESCO
mkoa wa Lindi, Sotco Nombo amesema tarehe 15 mwezi huu wataanza
kusambaza vifaa katika kijiji cha Chinongwe na kwamba hadi kufikia mwezi
Mei mwaka huu umeme utakuwa umewaka katika kijiji hicho.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu, Majaliwa amewasisitiza wananchi kuanza kulima kwa wingi zao la
muhogo kwa sababu kuna soko la uhahika la zao hilo baada ya kujitokeza
kwa wafanyabiashara kutoka China na Marekani wanaotaka kununua zao
mihogo nchini.
“Mnataka hela, mnataka hela? ila
lazima mfanye kazi…mimi nimewatafutia hela nawaomba mlime mihogo kwa
wingi maana kuna wafanyabiashara wanataka kununua mihogo, hela ndiyo
hiyo ambayo ni soko la uhakika la mihogo. Nawasihi mchangamkie dili
hili,” amesema.
Amesema wafanyabiashara hao
wanataka kununua mihogo kutoka wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale
kwa ajili ya kusaga unga na kutengeneza vyakula vingine vitokanavyo na
zao hilo, hivyo amewaomba wananchi hao kuchangamkia fursa hiyo na kulima
mashamba makubwa ya mihogo.
0 maoni:
Chapisha Maoni