TIMU ya soka ya Uchukuzi Sports Club ikiwa katika picha ya pamoja wakati wa mazoezi.
Wachezaji wa timu ya soka ya Uchukuzi Sports Club wakifanya mazoezi.
…………………………………………………………………………………………………………………
TIMU ya soka ya Uchukuzi Sports
Club mwishoni mwa wiki ilitoka sare ya kufungana bao 1-1 na Amadori Boys
ya Pugu Sekondari katika mchezo wa kirafiki uliofanyika jirani na
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Uchukuzi Sports Club inajiandaa
kwa mashindano ya Mei Mosi yatakayoanza Aprili 16 mkoani Dodoma, ambapo
mechi hiyo ni ya pili ya majaribio baada ya ile ya kwanza iliyofanyika
hivi karibuni.
Katika mchezo huo, Uchukuzi SC
ndio walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Isack Ibrahim katika
dakika ya saba kabla ya Christian Moyo hajasawazisha mwanzoni mwa
kipindi cha pili.
Hatahivyo, Ibrahim alikosa magoli
kadhaa ya wazi, baada ya walinzi wa Amadory Boys kumkaba baada ya kuona
ni tishio langoni mwao.
Meneja wa Uchukuzi SC, Robert
Damian aliyewahi kuichezea Simba ya Jijini Dar es Salaam, alisema kuwa
mechi hizo za kirafiki zinawasaidia makocha wa timu yao kujua makosa ya
wachezaji wao na kuyarekebisha kabla ya kwenda kwenye kituo cha
mashindano, ili waweze kufanya vizuri.
Alitamba kuwa timu yao ya soka
pamoja na nyingine za netiboli, kuvuta kamba, riadha, bao, drafti na
vishale zitafanya vizuri katika mashindano hayo ya Mei Mosi kwani
zimejiandaa vizuri, kwa kupata mechi kadhaa za kirafiki.
Aidha, timu ya netiboli ya
Uchukuzi SC juzi ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bandari Kurasini huku
ikiwa na wachezaji wake wakongwe kama akina Matalena Mhagama, Subira
Jumanne, Fanuna na wengineo, ambao wanaipa nguvu timu hiyo chini ya
kocha wao mzoefu Judith Ilunda.
Timu ya Uchukuzi SC katika
mashindano yaliyopita ya Mei Mosi yaliyofanyika jijini Mwanza, iliweza
kutwaa makombe 13, kati ya hayo matano ni ya ubingwa katika michezo ya
kuvuta kamba, baiskeli, bao, karata na riadha kwa upande wa wanawake na
wanaume, wakati yaliyosalia ilishika nafasi ya pili na tatu.
0 maoni:
Chapisha Maoni