Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiiano Profesa Makame Mbarawa amesema
Serikali haitaongeza muda katika zoezi zima la uzimaji wa simu feki
ifikapo Juni 16 mwaka huu.
Ameyasema hayo ofisini kwake leo jijini Dar es salaam wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha habari hapa nchini .
Amesema Serikali imeamua kuchukua
uamuzi huo kutokana na madhara mbalimbali yatokanayo na simu hizo
ikiwemo ya kiafya na kusisitiza kuwa serikali inapoteza mapato mengi
kutokana na uingizwaji wa simu hizo nchini.
‘Tunategemea kuzima simu zote feki
kutokana na madhara yake kiafya hasa kwa watumiaji, kukosekana kwa
viwango vya ubora wa simu hizi na hivyo wananchi kupoteza fedha nyingi
kwa ajili ya ununuzi wa simu hizi kwani hufa mara kwa mara’, amesema
Waziri Mbarawa.
Aidha, Profesa Mbarawa ameongeza
kuwa kwa sasa Jopo la wataalamu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) limepelekwa mkoani Singida kwa ajili ya kutoa elimu ya utambuzi
wa simu hizo ili kuweza kuwasaidia wananchi kubaini kwa urahisi.
Amesisitiza wananchi kuchukua
tahadhari kabla ya kununua simu ikiwemo kumuuliza muuzaji kabla ya
kununua, kudai risiti na kuituinza ili kudhibiti uingizwaji na
usambazaji wa bidhaa hizo nchini.
Katika hatua nyengine, Waziri
Mbarawa amesema kuwa suala la mkongo wa Taifa linaendelea vizuri ambapo
Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano wanaendelea na
usimikaji wa minara ya mawasiliano katika sehemu mbalimbali za nchi
hususan vijijini ili kuleta huduma bora za mawasiliano nchini.
‘Kwa sasa awamu ya nne ya mradi
huu wa Mkongo wa Taifa unaendelea, kwani makampuni mbalimbali ya simu
yanasimika minara yao katika sehemu mbalimbali za nchi ili kusambaza na
kuboresha mawasiliano kwa wananchi’, amefafanua Profesa Mbarawa.
Ameongeza kuwa uwepo wa mkongo
huo nchini kumepelekea mapinduzi katika sekta ya mawasiliano, mabenki na
kuiongezea Serikali pato kwani hata nchi za jirani hutumia mkongo huo
katika kupata mawasiliano yaliyo bora.
Tathmini imebainisha kuwa kutokana
na uwepo wa mkongo huo nchini watumiaji wa simu wamefikia milioni 39.7
na wa intaneti kufukia milioni 17.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi)
0 maoni:
Chapisha Maoni