———————————————
Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) Bw. Mohamed Kiganja ameitaka Kamati ya Oliympiki
Tanzania (TOC) wajiulize na kujifunza jinsi nchi zingine zinavyokuza na
kuendeleza michezo kupitia kamati hizo.
Rai hiyo ameitoa leo wakati
akifungua mafunzo ya Ualimu wa Mpira wa Meza yanayofanyika kwa siku nane
kuanzia tarehe 4 hadi 11 Julai mwaka huu katika Shule ya Msingi Kisutu
jijini Dar es salaam.
Aidha, ameitaka Kamati hiyo kuweka
wazi kwa vyama mambo wanayotakiwa kuyafanya kuendeleza michezo
wanayoelekezwa na Kamati ya Olimpiki ya dunia.
“TOC jengeni mahusiano yakaribu na
muwe wawazi kwa vyama, mpo kwa ajili ya kuendeleza michezo, fanyeni
vile mnavyoelekezwa na Kamati hii duniani”, alisema Kiganja.
Katika hatua nyingine Kaimu Katibu
Mkuu wa Baraza Bw. Mohamed Kiganja amekielekeza chama cha mchezo wa
meza kupanua wigo kwa kuanzisha vituo vingine katika Manispaa za
Kinondoni na Temeke na katika shule tofauti za Mkoa wa Dar es salaam na
wasitegemee kituo kimoja cha shule ya Kisutu pekee.
Aliendelea kuwa, chama hakina budi
kwenda mbali zaidi katika Mikoa mingine ambapo, aliwahakikishia kuwa,
Baraza liko tayari kuwasaidia kwa Makatibu Tawala ili kuona mchezo huo
unakuwa katika Mikoa yote nchini.
“Tuwatengenezee mazingira Walimu wanaopata mafunzo”, alieleza.
Awali Kaimu Mwenyekiti wa Chama
cha Mpira wa Meza (TTTA) Bw. Athony Mutafurwa ameeleza changamoto
zinazokikabili chama cha mpira wa meza ni pamoja na Uwanja na fedha
ambapo ameeleza kuwa, TTTA inaishauri Serikali kurudisha mfumo wa kutoa
ruzuku kwa vyama na kuongeza kuwa:
Serikali ione umuhimu wa kujenga
uwanja wa ndani wenye hadhi ya kimataifa katika awamu ya pili ya ujenzi
wa uwanja wa Taifa ili Tanzania tuweze kuandaa mashindano ya kimataifa
ambayo yamekewa yakishindikana kutokana na kukosekana kwa uwanja.






0 maoni:
Chapisha Maoni