Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
amewaasa watanzania kudumisha amani iliyopo ambayo ilipatikana baada ya
Mashujaa mbalimbali kuipigania na hata kujitoa uhai wao kwa ajili ya
Taifa.
Akizungumza
leo, wakati akihutubia wananchi mara baada ya kumaliza shughuli za
maadhimisho ya Siku ya kumbukumbu ya Mashujaa iliyofanyika katika
viwanja vya Mashujaa vilivyopo mjini Dodoma.
Rais
Magufuli alisema kuwa maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa ni muhimu
kwa vile watu hao walijotoa kwa ajili ya kulitetea taifa.
“Wakati
tunawakumbuka waliotangulia mbele za haki, sisi tuliobaki tudumishe
amani hii, kama ambavyo wao waliotutangulia hawakujali dini zao bali
taifa hili,” alisema Rais Magufuli.
Aliongeza
kuwa nchi ya Tanzania imebaki kuwa kisiwa cha amani, na amani hiyo
isichezwe bali ijengwe na kudumishwa kwa umoja na mshikimamano ili
kusaidia kuitangaza nchi zaidi.
Aidha,
viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, Mheshimiwa Dkt.Ali Mohamedi Shein, Rais Mstaafu wa Awamu ya
Pili Mheshimiwa Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu Mstaafu
Mheshimiwa John Samweli Malecela nao wapewa fursa ya kuzungumza na
wananchi kuhusu maadhimisho hayo ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa.
Viongozi
hao, wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani iliyopo na kusema kuwa ni
jukumu la wananchi wote kuhakikisha hawashiriki katika vitendo
vitakavyosababisha uvunjifu wa amani.
Ambapo,
waliwataka wananchi kuwaombea Mashujaa wote waliofariki katika vita
mbalimbali wakiwa katika harakati za kulifanya Taifa la Tanzania kuwa
huru.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alisema kuwa
atahakikisha anasimamia utekelezaji wa agizo la Rais la kuitaka Serikali
kuhamia mjini Dodoma.
“Nahamia
Dodoma mwezi wa tisa,na nitakapohamia mawaziri wote lazima wanifuate.
Katika hili nitasimamia kwa nguvu zote,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Awali,
Mheshimiwa Rais Magufuli alisema kuwa atahakikisha katika kipindi cha
utawala wake, Serikali inahamia mjini Dodoma, kwa vile Rais wa Awamu ya
kwanza Mwl. Julius Nyerere alionesha nia ya kufanya hivyo.
Aliongeza
kuwa kwa sasa mji wa Dodoma unaweza kukidhi mahitaji hayo ya Serikali
kwa kutumia miundombinu iliyopo, hata hivyo Serikali inaendelea kujenga
miundombinu mipya.
Maadhimisho
ya kumbukumbu za Mashujaa hufanyika Julai 25, ya kila mwaka, kwa
kufanya maombolezo ya Mashujaa waliopigana katika vita mbalimbali katika
harakati za kutetea uhuru wa nchi ya Tanzania.
Maadhimisho
ya mwaka huu yamefanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma, ambapo Rais
John Pombe Magufuli alikuwa mgeni rasmi, ikiwa ni mara yake ya kwanza
kuhudhuria maadhimisho hayo kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
0 maoni:
Chapisha Maoni