Postedy byEsta Malibiche on July 25, 2016 in BIASHARA with No comments
Dar es Salaam
SERIKALI imesema sekta ya
kilimo inaendelea kuwa sekta muhimu katika uchumi wa Tanzania kwa
asilimia 25% ya pato la taifa na kuajiri asilimia 75% ya watanzania
wakiwemo wanawake na vijana.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano katika Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Richard Kasuga wakati wa uzinduzi wa mchezo wa redio uitwao
KUMEKUCHA unaotarajia kuonyesha mchango wa wanawake na vijana katika
kutokomeza tatizo la uhaba wa chakula nchini.
Kasuga amesema kuwa
igizo hilo la mchezo wa redio, litaakisi umuhimu wa ushirikishwaji wa
wanawake na vijana katika kukuza sekta ya kilimo na kutoa ujumbe kwa
vijana kuona umuhimu wa kilimo hasa kilimo cha biashara.
“Sheria na tamaduni zilizopo
zinakwaza juhudi za mwanamke kupata fursa za kiuchumi kwa sababu hawana
haki ya kumiliki ardhi au vifaa vya kilimo, vyanzo endelevu vya maji,
ukosefu wa mikopo ambayo wanahitaji ili kufanikisha juhudi zao”alisema
Kasuga.
Kwa upande wake mwakilishi
kutoka shirika la msaada la Marekani (USAID) Randy Chester alisema kuwa
mchezo wa KUMEKUCHA umeandaliwa na taasisi ya Africa Lead kwa
kushirikiana na Media for Development International (MFDI) na
kufadhiliwa na USAID kwa lengo la kupunguza uhaba wa vyakula vyenye
virutubisho hapa Tanzania.
Mchezo wa KUMEKUCHA ni mchezo
wa redio wa kila wiki ambao unaangazia maisha, vikwazo na fursa za
wakulima Tanzania na utaanza kurushwa hewani kuanzia Julai 25, 2016
kupitia Redio Free Afrika, Redio Abood FM, Redio Ebony FM na Redio Bomba
FM.
0 maoni:
Chapisha Maoni