Jumatatu, 25 Julai 2016

WAZIRI WA KILIMO DK CHARLES TIZEBA ATUMBUA MAJIPU YA TUMBAKU TABORA

tiz1*Na Paul Christian,Tabora*
Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi  Injinia Dkt. Charles Tizeba amefanya ziara ya kikazi mkoani Tabora kwa lengo la kubaini changamoto zinazolikabili zao la tumbaku.
Katika ziara hiyo waziri huyo  ametembelea masoko ya zao hilo yaliyofanyika kwenye vyama vya msingi vya ushirika wa wakulima wa tumbaku vya Tumbi katika manispaa ya Tabora na Ngulu wilayani Sikonge.
Akiwa kwenye masoko hayo ameweza kuzungumza na wakulima,wateuzi (classifiers) , wanunuzi (blenders),viongozi wa vyama vya ushirika, wajumbe wa bodi ya tumbaku Tanzania (TTB).
Akifanya majumuhisho ya ziara hiyo mbele ya wadau wa zao hilo kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora *Dkt Tizeba ameagiza yafuatayo:-*
Makampuni yanayonunua  tumbaku mkoani Tabora kuwalipa wakulima malipo yao ya pili bila masharti ya miti.
Bodi ya Tumbaku kufanya hesabu ya kilo zilizokuwa zikikatwa na makampuni yanayonunua zao hilo kwa kile kinachodaiwa “mnyauko” ambao unaosababisha uzito wa tumbaku kupungua kwa kuwa mnunuzi amechelewa kuondoa Tumbaku yake kwenye Magodauni baada ya kuinunua, baada ya hesabu hiyo makampuni yatawalipa wakulima kwa msimu huu na misimu mingine iliyopita.
Mabenki yote yaandike mikataba yote kwa lugha ya Kiswahili ili wakulima waweze kuielewa mikataba hiyo.
Mabenki kuacha kuwaibiwa wakulima kwa kucheza na ubadilishaji fedha kutoka dola ya kimarekani kwenda kwenye shilingi ya Tanzania.
Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuhamisha makao yake makuu kutoka Morogoro hadi mjini Tabora.
Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuacha kuburuzwa na makampuni yanayonunua Tumbaku au Tobacco Council na badala yake wasimamie sheria kikamilifu.
Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB kuanzia msimu ujao wa masoko ifute kabisa matumizi ya mizani ya rula na aina zake zote na badala yake itumike mizani ya electronic ili kuandoa wizi kupitia mizani.
Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB ipunguze madaraja ya Tumbaku kutoka 72 ya sasa.
Mabenki kuacha kuyaingiza makampuni ya ununuzi wa Tumbaku kwenye mikataba ya mikopo kwenye vyama vya msingi.
Mrajis wa vyama vya Ushirika nchini kuhakikisha vyama vya msingi ahakikishe vyama vya Ushirika 105 kati ya 217 vilivyoko hatarini kufutwa mkoani Tabora vinarejea kutoa huduma kwa wanachama wao badala ya kuvifuta.
Mrajis atapoteza ajira yake ikibainika chama cha Ushirika au SACCOS imekufa.
Kuanzia msimu ujao Chama Kikuu Cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi WETCU LTD hakita endeshwa na fedha ya makato ya moja kwa moja kutoka kwenye kila kilo ya tumbaku na badala yake wataomba fedha kutoka vyama vya msingi ambavyo ni mwanachama wa WETCU LTD na sio mkulima mmoja mmoja.
Halmashauri ya Tumbaku (Tobacco Council) sio chombo cha kisheria hivyo kisitumike kumkandamiza mkulima.
Mkulima hatokatwa kilo moja (mara mbili) kwa ajili ya uzito wa gunia analofungia tumbaku.
Ni mara ya kwanza na ya mwisho kwa mtendaji mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania kushindwa kufika kwenye ziara ya waziri mwenye dhamana.
Independent Famers (IF) na Association ni marufuku kwa kuwa zilitumika kuua ushirika.
Wakulima waache kuchanganya grade tofauti za tumbaku kwenye mtumba mmoja.
Wakulima wadhibitiwe kutorosha tumbaku.
Kwenye vyama vya Msingi akopeshwe mkulima mmoja mmoja na sio kwa vikundi ili kila mmoja abebe mzigo wa kulipa deni lake.
Waziri Tizeba amebaini yafuatayo katika ziara hiyo:-
Uchaguzi wa viongozi kwenye vyama vya Ushirika ni Vita kuliko hata kugombea Ubunge.
Tumbaku haijabadilisha maisha ya watu.
Asilimia 90 ya matatizo yaliyoko kwenye vyama vya msingi vya ushirika yamesababishwa na watu walioko nje ya vyama hivyo na asilimia 10 ni wanachama wa vyama hivyo.
Kwenye masoko wanunuzi (Blenders) wanasauti kuliko wateuzi wa serikali (classifiers).
Maofisa ushirika ni chanzo cha kufa kwa vyama vya Ushirika.
Mrajis ni chanzo cha kufa kwa vyama vya ushirika kwa kuwa anaidhinisha mikopo, utoaji fedha,bajeti na nk.
Mabenki ni chanzo cha kufa kwa vyama vya ushirika yanatumia uelewa mdogo wa wakulima kujinufaisha kwa wizi.
Bodi ya Tumbaku Tanzania TTB ni chanzo cha kuua ushirika kwa kuwa imeshindwa kutimiza wajibu wake.
Tobacco Council inaamua kila kitu na sio Bodi ya Tumbaku Tanzania.
Viongozi wa vyama vya msingi wanaingia mikataba wasiyoijua au kuielewa.
Mikopo ya mabenki imekatiwa bima lakini vyama vya msingi vikishindwa kulipa mikopo hiyo bado wanaendelea kudaiwa.
Zabuni za usambazaji Pembejeo zinatolewa kwa misingi ya Rushwa.
Bei ya mbolea inayonunuliwa kwa jumla ni kubwa kuliko bei ya rejareja.
Kwenye soko kuna madaraja 72 ya tumbaku ambapo tumbaku hiyo hiyo ikifika kiwandani Morogoro kuna kitu kinaitwa “inhouse grading” inayotoa madaraja zaida ya 100 yasiyohusiana na madaraka yanayotumika kwenye soko.
Mabenki yamevikopesha Vyama vya msingi AMCOS ili vijenge Maghala huku wakandarasi wakiwekwa na Mabenki hayo hayo baadhi ya Maghala hayajakamilika na Mabenki yanaendelea kukata fedha za Wakulima kulipa mkopo.

0 maoni:

Chapisha Maoni