Mstahiki Meya wa mji wa Dodoma Jaffari Mwanyemba, amesema kuwa watanzania wanatakiwa kuwaenzi Mashujaa waliopigana katika vita mbalimbali ikiwa ni katika harakati za kuiletea uhuru nchi ya Tanzania.
Hayo yamesemwa leo saa sita usiku, wakati alipokuwa akizima Mwenge wa uhuru uliowashwa jana Julai 24, na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mheshimiwa Christina Mndeme katika kilele cha mnara wa mashujaa mnano saa 6 kamili usiku ikiwa ni sehemu ya maombolezo ya kumbukumbu ya Mashujaa, yaliyofanyika katika Uwanja wa Mashujaa uliopo mjini Dodoma.
“Watanzania tuna jukumu la kuwaenzi Mashujaa kwa kufanyakazi kwa bidii, nidhamu na uadilifu, na kama wote tutafanya hivyo tutakuwa tumewaenzi mashujaa wetu” alisema Mstahiki Meya Mwanyemba
Ameongeza kuwa kila mwananchi atimize uwajibu wake kwa kufanyakazi, ili kila mmoja atapata haki yake na hivyo kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini.
Maadhimisho ya kumbukumbu za Mashujaa kwa mwaka huu yamefanyika leo julai 25, mkoani Dodoma ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.