TANZANIA
imeuhakikishia Umoja wa Afrika (AU) kwamba itaendelea kufanya kazi kwa
karibu na nchi wanachama wa umoja huo, kujadili changamoto za kiusalama
zinazolikabili bara la Afrika, kwa njia ya mazungumzo na upatanishi,
kama inavyoelekeza Katiba ya AU.
Makamu
wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada
kuhusu hali ya amani na usalama katika bara la Afrika, kwenye Mkutano wa
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika mjini
Kigali, Rwanda.
Samia
alisema Tanzania inasikitishwa na inalaani matukio ya uvunjifu wa amani
yanayoendelea kujitokeza katika baadhi ya nchi za Afrika kiasi cha
kutishia usalama wa raia.
Alielezea
mauaji ya Hafsa Mossi aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki
(EALA) na Waziri wa zamani wa Burundi na mapigano ya hivi karibuni Sudan
Kusini ambako mamia ya raia wasiokuwa na hatia waliuawa na wengine
maelfu wameachwa bila makazi, kwamba ni mwendelezo wa uvunjifu wa amani
katika nchi hizo.
Aliwataka
wadau husika katika nchi za Burundi na Sudan Kusini kushiriki
kikamilifu katika mazungumzo yanayoendelea kwa kuwa hiyo ndiyo njia
muafaka ya kuleta amani, usalama na utulivu wa kudumu katika nchi zao.
Aidha,
aliiomba Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuisaidia Sudan Kusini kutafuta
ufumbuzi wa kudumu katika mgogoro ulioikumba nchi hiyo.
Akichangia
kuhusu mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Makamu wa Rais
alisema Tanzania kwa ujumla inaunga mkono msimamo wa Afrika wa kuwa na
viti viwili katika baraza hilo na kura ya turufu bila ya masharti
yoyote.
0 maoni:
Chapisha Maoni