Wasanii nchini wameaswa kuzingatia maaadili katika utengenezaji wa kazi zao ili kuenzi na kulinda mila, desturi na tamaduni za mtanzania .
Wito huo umetolewa jana na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura wakati akizindua studio ya kisasa ya kurekodi kazi za sanaa ya Wenene Entertainment.
Mhe Anastazia Wambura amesema kuwa baadhi ya wasanii wamekuwa hawafati maadili katika utengenezaji wa kazi zao na kuvifanya vyombo vinavyosimamia kazi za sanaa nchini kama Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kutoa adhabu dhidi yao kutokana na ukiukwaji wa maadili katika kazi zao.
“Ninaiomba kampuni ya Wanene Entertainment kuisaidia Serikali kuwaelimisha wasanii watakaoleta kazi zao kutengenezwa kwenu kuzingatia maadili badala ya kutengeneza kazi ambazo haziendani na maadili ya nchi yetu” alisema Mhe Anastazia.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bibi. Joyce Fissoo amehaidi kushirikiana na studio ya Wanene Entertainment kuendeleza sanaa ya Tanzania kufikia katika viwango vya kimataifa na kuongeza pato la wasanii na taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Wanene Entertainment Bw. Darsh Pandit amesema kuwa ufunguzi wa studio hiyo ni muitikio wao kwa Serikali ya awamu ya tano katika suala la kutoa ajira kwa vijana na kuwezesha vijana kujiajiri kwa kutumia vipaji vyao kupitia kazi za sanaa.
“Studio hii ina lengo la kukuza na kuendeleza sanaa ambayo imekuwa ajira kubwa kwa vijana wengi na tunaahidi kuzingatia maadili katika utengenezaji wa kazi zetu na pia tutazingatia ubora ili kuitangaza sanaa ya Tanzania kimataifa” alisema Bw. Pandit.