Jumanne, 26 Julai 2016

Kambi kuu ya Amisom yavamiwa Mogadishu


Washambuliaji wa kujitoa mhanga wameshambulia kambi kuu ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika (AU) mjini Mogadishu.
Milipuko miwili mikubwa imesikika karibu na lango la kambi hiyo ifahamikayo kama Halane na baadaye kukatokea ufyatuaji wa risasi.
Makao makuu ya wanajeshi hao yamo karibu na uwanja wa ndege wa Mogadishu, eneo ambalo pia lina afisi nyingi za ubalozi za mataifa ya Magharibi na Umoja wa Mataifa.
Mlipuko wa kwanza ulipasua vioo vya majumba katika uwanja wa ndege.
Taarifa zinasema mshambuliaji wa kwanza alilipua bomu lililotegwa kwenye gari na wa pili akajaribu kuingia ndani ya kambi hiyo kwa miguu lakini akapigwa risasi na akalipuka akiwa karibu na lango.
Shirika la habari la Reuters linasema watu saba wamefariki.


Kundi la al-Shabab limedai kuhusika, na kusema watu zaidi ya 12 wameuawa kwenye shambulio hilo. Msemaji wa kundi hilo ambaye ametambuliwa kama Abdiasis Abu Musab amesema washambuliaji wote wawili walilipua mabomu ya kutegwa kwenye magari.

0 maoni:

Chapisha Maoni