Postedy by Esta Malibicheon July 27, 2016 in JAMII with No comments
Picha na Hassan Silayo-MAELEZO
……………………………………………………………………………………………………………..
Na Hassan Silayo-MAELEZO
Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sihaba Nkinga amewataka
watanzania hasa vijana wenye uwezo, wanaopekea na kukaa na wazee wao
kwenye kambi za kulea wazee kuacha mara moja tabia hiyo.
Akiongea wakati alipotembelea
kambi ya kulea ya wazee ya Sukamahela iliyopo Wilayani Manyoni Mkoani
Singida Bi. Sihaba alisema kuwa Serikali itaanza kuwachukulia hatua
za kisheria watanzania wenye tabia hiyo kwani kufanya hivyo ni kukiuka
sheria ya wenye ulemavu na wazee inayowataka wanafamilia kuwa na jukumu
la kwanza la kumlea mzee na mtu mwenye ulemavu.
“Kumekuwa na utamaduni kwa baadhi
ya vijana nchini kupeleka wazee kwenye hizi kambi za kulea wazee huku
vijana hao wakionekana na kuwa na uwezo wa kuwalea, kwa kweli huu
utaratibu sisi kama serikali hatuwezi kuuvumilia kwanza ni ukiukwaji wa
sheria ya watu wenye ulemavu na wazee inayowataka wana familia kuwa na
jukumu la kuwalea wazee, hivyo ni matarajio yetu kuwa kijana amlee mzee
wake kama alivyolelewa yeye, Sisi kama serikali tutachukuwa jukumu la
kuwalea wazee na watu wenye ulemavu wanaotoka kwenye familia zisizo na
uwezo kabisa”. Alisema Bi. Sihaba.
Bi. Sihaba aliongeza kuwa
utamaduni huo pia unawanyima fursa Wazee na watu wenye ulemavu wanaotoka
kwenye familia zisizo na uwezo kupata huduma kutokana na baadhi ya watu
kukwepa majukumu yao ya kifamilia wakati wanauwezo wa kufanya hivyo na
kuzifanya kambi hizo kujaa na kushindwa kupokea watu wenye uhitaji.
Aidha, Bi. Sihaba alisema kuwa
Serikali ya awamu ya tano itaendelea kusimamia azma yake ya kuisaidia
wazee na watu wenye ulemavu nchini ili kuhakikisha inapunguza na kuondoa
kabisa changamoto zinazokabili kundi hilo.
Naye Afisa Mfawidhi wa Kambi hiyo
Bw. Jeremiah Paul ameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kuzisimamia
ipasavyo kambi hizi kwani itasaidia kuondoa kabisa changamoto
zinazowakabili Wazee na watu wenye ulemavu katika maeneo hayo.
Akizungumza kuhusuutoaji huduma
za Afya kwa Wazee wa Kambi hiyo Muuguzi wa Zahanati ya Serikali ya
Sukamahela iliyokaribu na Kambi hiyo Bi Marry Sailale ameishukuru
serikali kwa kuona umuhimu wa kujenga zahanati hiyo karibu na kambi ya
Wazee na kuomba kuongezewa vifaa na wafanyakazi katika zahanati hiyo ili
kuongezea ufanisi katika kuwahudumia wazee wanaohitaji uangalizi wa
karibu.
0 maoni:
Chapisha Maoni