…………………………………
SERIKALI iko mbioni kutoa
hatimiliki zaidi ya 25,000 kwa wakazi wa kata za Kimara na Saranga
zilizopo jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kurasimisha makazi
holela.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Mratibu wa Mradi wa urasimishaji wa makazi holela Kata za
Kimara na Saranga, Bi Grace Masatu wakati wa zoezi la ukaguzi wa maeneo
ya mradi.
“Zoezi za la upimaji linaenda
sanjari na utambuzi wa mipaka,ujazaji wa madodoso, uchoraji wa ramani za
upimaji na mipangomiji,”alisema Masatu.
Viwanja zaidi ya 25,000
vinatarajiwa kupimwa katika kata za Kimara na Saranga ambapo hadi leo
ramani za upimaji 14 na ramani sita (6) za mipangomiji zenye jumla ya
viwanja1028 ziko tayari na zimeshawasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kwa ajli ya kupitishwa, alisema Masatu.
Aidha, Masatu amesema kuwa malengo
ya mradi huo ni kuongeza thamani ya makazi kwa kutoa hatimiliki na
kutambua mipaka ya wakazi wa maeneo husika.
Kwa upande wake, Afisa Mipango
miji Mkuu, Bi Anna Macha, alisema kuwa hadi sasa maeneo yaliyopimwa
katika kata ya Kimara ni mtaa wa Kilungule A wote pamoja na viwanja 724
vya mtaa wa Kilungule B, ambavyo vimechukuliwa mahesabu ya upimaji kwa
ajili kuandaa ramani.
Ameongeza kuwa umetengenezwa mfumo
maalum ambao unachukua taarifa za madodoso zinazojazwa wakati wa
utambuzi wa mipaka ya wamiliki wa maeneo husika. Mfumo huo utaunganishwa
na mfumo wa Kamishna wa Ardhi (MOLIS) utakaorahisisha kufahamu idadi ya
viwanja vilivyopimwa na kumilikishwa.
Naye Mjumbe wa Mtaa wa Kilungule
B, Bwana Claud Misri Silayo ameonyesha kuridhishwa na zoezi zima la
utambuzi na upimaji wa maeneo.
“ Nimefurahishwa na zoezi la
upimaji kwani nitamiliki ardhi kisheria, kihalali na nitafaidika na
ardhi ninayomiliki kwa sababu mwisho wa zoezi hili nitapata hatimiliki
ambayo itaniwezesha kupata mikopo kwenye taasisi za fedha,”alisema
Silayo.
Urasimishaji ni mwendelezo wa
utambuzi wa makazi holela katika jiji la Dar es Salaam unaotekelezwa
chini ya Sheria ya Ardhi Na. 4 pamoja na Sheria ya Mipangomiji.
0 maoni:
Chapisha Maoni