Watu
watatu wamefariki dunia mkoani Singida, katika matukio tofauti likiwemo
la mzee mmoja aliyepoteza maisha baada ya kutokwa na damu nyingi
kutokana na kufanyiwa upasuaji wa tezi dume na daktari feki.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa
wa Singida, ACP Thobias Sedoyeka, alimtaja mzee huyo aliyefanyiwa
upasuaji wa tezi dume, kuwa ni Israel Shaban (68) mkazi wa kijiji cha
Kinyambuli kata ya Nkinto tarafa ya Kirumi wilaya ya Mkalama.
Alisema
Julai, 14 mwaka huu saa mbili usiku mzee Shaban alienda nyumbani kwa
Joseph Msafiri anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 na 40 ambaye
alikuwa ameigeuza nyumba yake kuwa ni kituo cha kutolea huduma za afya.
Akifafanua, alisema inadaiwa kuwa Joseph katika miaka ya nyuma aliwahi kuwa mwajiriwa wa serikali kwa nafasi ya utabibu.
Kamanda
Sedoyeka alisema kutokana na uzoefu huo, baada ya kuacha kazi
serikalini, huku akijiita ni daktari, aliamua kuanza kutoa tiba ikiwemo
upasuaji nyumbani kwake kinyume na sheria.
“Mtuhumiwa
baada ya kumfanyia upasuaji huo wa kienyeji Mzee Shaban katika sehemu
zake za siri, alitokwa damu nyingi na kupelekea kuwa katika hali mbaya.
Mtuhumiwa alipobaini hali hiyo, alimtekelekeza na kufanikiwa kutoroka na
kukimbilia kusiko julikana. Kwa sasa tupo kwenye msako mkali ili
kumkamata na kumfikisha mahakamani,” alisema.
Aidha,
alisema baada ya kufanya upekezi kwenye nyumba ya dakatari feki huyo,
wamefanikiwa kukamata vifaa vingi vya utabibu na dawa nyingi za kutibu
binadamu.
Katika
tukio jingine, Kamanda Sedoyeka alisema Julai, 17 mwaka huu saa tano
asubuhi, Hamisi Salum (24) mkazi wa kijiji cha Misuna wilaya ya Mkalama,
amemwua mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Mgungira wilaya ya
Iramba, Sharifa Juma (12), kwa kumkata kwa panga kichwani na shingoni.
Alisema
chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa muda mrefu kati ya marehemu na
mtuhumiwa uliosababishwa na kitendo cha baba wa mtuhumiwa kumpendelea
kwa kila kitu huku Sharifa (marehemu) akiwa ni mtoto wa kambo.
“Kwa
sasa tunamshikilia Hamisi kwa mahojiano zaidi na baada ya kukamilika
kwa mahojiano hayo, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma ya
mauaji,” alisema.
Wakati
huo huo, Sedoyeka alisema Julai, 16 mwaka huu saa 12 jioni huko mtaa wa
Karakana mjini hapa, mwili wa Patrick John (34) mkazi wa Karakana
uliokotwa barabarani baada ya kutupwa.
“Chanzo cha mauaji bado kinaendelea kuchunguzwa na hakuna mtu au watu waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo,” alisema Sedoyeka.
Imeandikiwa na Nathaniel Limu, Singida
0 maoni:
Chapisha Maoni