Postedy by by Esta Malibiche on July 22, 2016 in JAMII with No comments
………………………………………….
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Bi.
Maimuna Tarishi ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la
Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kufuta programu zinazotolewa na vyuo
vikuu hapa nchini ambazo hazijafanyiwa tathmini wala kusajiliwa.
Katibu
Mkuu huyo ameyasema hayo leo alipokuwa akifunga maonyesho ya kumi na
moja ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyoanza Julai 20 katika
viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
“Wakati
mwingine najiuliza inakuwaje chuo kinafundisha programu ambayo
haijatathminiwa wala kusajiliwa na TCU au NACTE, ni lazima tuwe makini
kwani tunahitaji elimu bora katika vyuo vyote nchini bila kuangalia kama
ni cha Serikali au ni Binafsi,” alifafanua Bi. Tarishi.
Aliendelea
kwa kusema kuwa, TCU na NACTE wanajukumu ya kuzifuta programu hizo na
kuanzisha programu zenye uhitaji mkubwa kama vile shahada ya mafuta na
gesi, Kompyuta na Ualimu wa Sayansi ambapo wataalamu katika maeneo hayo
wamekuwa wakihitajika zaidi katika kipindi hiki ambacho Serikali ya
Awamu ya Tano inajikita zaidi katika uanzishwaji wa viwanda.
Aidha
Bi. Tarishi amewataka TCU na NACTE kudahili wanafunzi wenye vigezo
vinavyohitajika na kusisitiza kuwa ni bora kuwa na wanafunzi wachache
katika vyuo vikuu kuliko kuwa na wanafunzi wengi ambao hawana sifa.
Wakati
huo huo Mkuu wa Kitivo cha Biashara Chuo Kikuu cha Zanzibar Salehe
Mwinyi amesema kuwa wanafunzi wengi wamejitokeza kutembelea banda la
Chuo hicho kutaka kujua pogramu zinazotolewa na wengi wao wameonyesha
nia ya kujiunga katika Chuo hiko.
Vile
vile Mwinyi amesema kuwa mwaka huu idadi ya wanafunzi waliotembelea
maonyesho hayo ni wengi zaidi kutokana na eneo lililochaguliwa kufikika
kwa urahisi kutoka pande zote za jiji la Dar es Salaam ukilinganisha na
mwaka jana ambapo yalifanyika viwanja vya Saba Saba na kutembelewa na
idadi ndogo ya wanafunzi na wazazi.
Kwa
upande wake, Fadia Suleiman mwanafunzi anayetegemea kujiunga na Chuo
Kikuu mwaka huu, amesema kuwa maonyesho hayo yamemsaidia kwa kiasi
kikubwa kujua ni programu gani asome kutokana na ufaulu wake wa kidato
sita.
Maonyesho
ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambayo huandaliwa na TCU
hufanyika kila mwaka yakitoa fursa kwa Vyuo Vikuu vya ndani na nje ya
nchi kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi wanaotegemea kujiunga na vyuo
vikuu kwa mwaka husika juu ya programu zinazotolewa na vyuo hivyo pamoja
na kutoa ushauri ni programu gani mwanafunzi asome kwa kuangalia ufaulu
wake.
0 maoni:
Chapisha Maoni