Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto)
akipata maelezo kutoka kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya simu
Tanzania (TTCL), jinsi ya mfumo wa kutoa taarifa kwa wafanyakazi
unavyofanya kazi wakati alipotembelea ofisini hiyo jijini Dar es salaam.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Dkt . Kamugisha
Kazaura akisoma taarifa ya utendaji kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Hayupo pichani) wakati alipoongea na
uongozi wa kampuni hiyo, jijini Dar es salaam.
Mwenyekiti
wa bodi ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Profesa Tolly Mbwete
akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa (hayupo pichani) wakati Waziri alipotembelea ofisi hiyo,
jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiongea na
Uongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wakati alipotembelea kampuni
hiyo, Jijini Dar es salaam.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Dkt . Kamugisha
Kazaura akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa wakati alipofanya mazungumzo na wafanyakazi wa
kampuni hiyo,jijini Dar es salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiongea na
wafanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL),Jijini Dar es salaam.
PICHA ZOTE NA BENJAMINI SAWE -MAELEZO
…………………………………………………………………………………………………..
Serikali imehitimisha ubia kati
ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), na Kampuni ya Bhart Airtel ya India
kwa kuilipa kampuni hiyo Shilingi Bilioni 14.9 na hivyo kuirudisha TTCL
mikononi mwa Serikali kwa asilimia miamoja.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hatua hiyo ni mkakati wa
Serikali wa kuiwezesha TTCL kujitegemea ili kuzalisha faida, Kuimarisha
Miundombinu yake, na kutoa gawio Serikalini.
“Tunawataka TTCL mjipange vizuri mjitangaze ili muwe kampuni kubwa na bora ya mawasiliano hapa nchini”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa amesema
katika kuiongezea nguvu TTCL Serikali itawapa kituo cha Kutunza Taarifa
cha Kijitonyama (Internet Data Center) ili ikisimamie na hivyo
kujipatia mapato kupitia gharama za uendeshaji na usimamizi wa kituo
hicho.
Amewataka wafanyakazi wa TTCL
kufanya kazi kwa bidii, kasi, uaminifu, ubunifu na kuulinda Mkongo wa
Taifa ili uwawezeshe kuwa na huduma bora na za uhakika wakati wote.
“Tumetumia fedha za mkongo wa
taifa kumlipa mbia mwenzenu bhart airtel ili kuiwezesha TTCL kumilikiwa
na Serikali kwa asilimia miamoja hivyo changamoto inayowakabili sasa ni
kufanya mabadiliko makubwa katika upande wa kutafuta masoko ili kuweza
kuongeza idadi ya wateja na kufanya kazi kwa faida”, amesisitiza Prof.
Mbarawa.
Aidha Prof Mbarawa amesema katika
kuijali TTCL, Serikali imeipa masafa ya 1800 na masafa ya 2100 na
itawaongezea masafa ya 800 yatakayowawezesha kuwa na huduma ya 4G LTE
yenye mtandao wenye kasi na hivyo kuiongezea wateja hususani katika
huduma za data.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Bodi ya TTCL, Profesa Tolly Mbwete amesema TTCL imejipanga kutoa huduma
zake katika maduka makubwa, hospitali, stesheni za treni, mabasi ya
mwendokasi na viwanja vya ndege katika jiji la Dar es salaam na Miji
mikubwa ili kuwawezesha wananchi kunufaika na huduma za mtandao na data
wakati wote.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TTCL Dkt.
Kamugisha Kazaura, ameishukuru Serikali kwa fursa mbalimbali inazoipa
kampuni hiyo na kumhakikishia Waziri Prof Mbarawa kuwa katika kipindi
cha miezi mitatu ijayo matokeo ya mkakati wa mabadiliko ya kibiashara
yataanza kuonekana.
Dkt. Kazaura amesema kuwa tayari
watumishi wenye mtazamo wa mabadiliko ya kiteknolojia wameajiriwa na
wengine watapewa mafunzo ili kuhimili soko la kibiashara na kuiwezesha
TTCL kunufaika na miundombinu yake iliyopo nchi nzima.
Waziri Prof. Mbarawa alikuwa
akizungumza na Menejimenti na wafanyakazi wa TTCL ikiwa ni utaratibu
aliojiwekea kuzungumza na wafanyakazi na taasisi zilizopo chini ya
Wizara yake.
0 maoni:
Chapisha Maoni