Ikiwa ni miezi nane tangu Jeshi la Polisi kukamata vifaa vya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa madai ya vifaa hivyo kutumika kutoa taarifa zisizo rasmi kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, hatimaye Polisi imerejesha vifaa hivyo kwa LHRC.
Katika taarifa ambayo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Helen Kijo-Bisimba imesema kuwa vifaa hivyo vilikamatwa Oktoba, 29 mwaka jana katika ofisi za Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Kuangalia Chaguzi Tanzania (TACCEO) zilizokuwa zikiratibiwa na LHRC kwa madai ya kuvunja kifungu namba 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Alisema Polisi walifika katika ofisi za TACCEO zilizopo Mbezi Beach na kuchukua vifaa vyao ambavyo ni kompyuta za mezani 24, kompyuta za mpakato 3, simu za mkononi 25 ambazo ni za ofisi na zingine za wafanyakazi na kuwakamata waangalizi wa kituo hicho 36.
“Polisi walifika katika kituo chetu kilichopo Mbezi Beach wakiwa na gari aina ya Land Rover difenda iliyokuwa na askari wakiongoza na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kipolisi Kawe, ASP Mgonja na baadae alifika Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es Salaam ndugu Salum na kuungana nao,” ilisema taarifa hiyo.
Aliongeza kuwa baada ya kuvichukua vitu hivyo pamoja na kuwakamata waangalizi waliwafikishwa kituo cha Polisi Kituo cha Polisi Kanda ya Kati na baadae kupelekwa Makao Makuu ya Polisi na baada ya kufanyiwa mahojiano waangalizi wote 36 walipatiwa dhamana na kutakiwa kuripoti tena Otoba, 30 kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano zaidi.
Alisema baada ya wiki mbili Polisi ilirudisha simu za binafsi za waangalizi wa kituo lakini hawakuwa tayari kurudisha vifaa vingine ndipo Mei, 3 ilipowasilisha Polisi notisi ya siku 90 na kama haitarudisha vifaa vyao basi wangewafikisha mahakamani.
Aidha wakati wakiwa wanasubiri siku hizo kumalizika, Julai, 15 walipokea taarifa kutoka Polisi ikiwataka kufika kuchukua vifaa vyao na Julai, 18 maafisa wa LHRC walifika Polisi na kukabidhiwa vifaa vyao vyote bila masharti yoyote lakini moja ya kompyuta zilizokamatwa ilikuwa imeharibika na baadhi ya waya za kumpyuta hiyo kushindwa kupatikana.