Ijumaa, 22 Julai 2016

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI

POLISIJeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu. Hata hivyo kuna matukio mawili ya mauaji yameripotiwa kutokea  katika wilaya za Chunya na Mbarali kama ifuatavyo.
Tukio la kwanza.
NEEMA NELSON MBUNGA [25], mfanyabiashara ya  mazao, mkazi wa Mengele – Chimala, aliuawa kwa kukatwa mapanga kichwani na mikononi akiwa amelala chumbani kwake.
Tukio hilo lilitokea tarehe 19.07.2016 majira ya saa 02:00hrs katika kijiji cha Mengele,  kata ya Chimala,  tarafa ya Ilongo wilaya ya Mbarali.   Watu wawili wanashikiliwa na Polisi kuhusiana na tukio hilo akiwemo kaka wa marehemu ANYAMISYE NELSON [34], mkazi wa Mengele – Chimala ambaye alikuwa amelala chumba cha pili katika nyumba hiyo ambayo haikuvunjwa sehemu yoyote na mtuhumiwa wa pili aliyekamatwa ni FREDY LUPONELO CHOTA [32], mkazi wa Chimala. Chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa. Begi dogo la marehemu limekutwa eneo la shule ya msingi Mengele umbali wa mita takribani 300 kutoka eneo la tukio likiwa na vitambulisho na nguo.
Tukio la pili.
Watu wawili  SHIJA MIGUDA [40] na mke wake KABULA KATABI [35], wakazi wa kitongoji cha Mpembe waliuawa kwa kukatwa mapanga mwilini wakiwa wamelala nyumbani kwao, baada ya mlango wa nyumba kuvunjwa.
Tukio hilo limetokea tarehe 19.07.2016 saa 02:30hrs kitongoji cha Mpembe, kijiji cha Mwiji, kata ya Lualaje, tarafa ya Kipembawe, wilaya ya Chunya. Chanzo cha tukio hili ni imani potofu za kishirikina kufuatia marehemu hao kutuhumiwa kuwa ni wachawi hapo kijijini. Watuhumiwa ambao ni majirani na marehemu walikimbia baada ya tukio, ufuatiliaji unaendelea.
WITO:
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi EMANUEL .G .LUKULA anatoa  wito kwa jamii hasa wahalifu kuacha tabia ya kuwa na  tamaa ya  utajiri wa haraka kwa kujipatia kipato  haraka kwa njia ya  mkato / haramu badala yake wajishughulishe kwa kufanya kazi halali na kupata kipato halali. Aidha Kamanda LUKULA anatoa rai kwa yeyote mwenye taarifa juu ya mtu / watu waliohusika katika matukio hayo  azitoe katika mamlaka husika ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake vinginevyo wajisalimishe mara moja. Pia anaendelea kutoa wito kwa jamii kuepukana na tabia ya kusadiki imani potofu za kishirikina kwani zina madhara makubwa kwa jamii ikiwemo kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
[EMANUEL G. LUKULA  – ACP]
KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

0 maoni:

Chapisha Maoni