Serikali kupitia Wizara ya
Nishati na Madini ambayo inatekeleza Mradi wa Usimamizi Endelevu wa
Rasilimali Madini (SMMRP) imetoa taarifa ya kukaribisha maombi ya Ruzuku
Awamu ya Tatu kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Akizungumza katika Kipindi cha
Jambo Tanzania kinachorushwa na Televisheni ya Taifa, TBC1, Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Madini, Profesa
James Mdoe alisema kuwa, kiasi cha ruzuku kilichotengwa kwa shughuli
hiyo ni Dola za Marekani Milioni Tatu.
Profesa Mdoe alisema kuwa,
taratibu zote za kupata washindi wa ruzuku hiyo zitafanyika kwa uwazi
huku zikishirikisha Vyama vya Wachimbaji vya Mikoa (REMA), lengo likiwa
ni kupata walengwa stahiki kutokana na kuwa, vyama hivyo vinawatambua
wanachama wao.
“Mbali na vyama vya wachimbaji,
pia Serikali itashiriki kupitia ofisi zetu za Kanda zilizoko katika
Mikoa yote kabla ya kufikishwa katika ngazi ya Wizara ambapo pia
kutakuwa na Kamati Maalum ya kushughulikia suala hilo,”alisisitiza Prof.
Mdoe.
Akizungumzia lengo la utoaji
ruzuku hiyo alisema kuwa, ni kukuza mitaji ya wachimbaji wadogo na
kuongeza kuwa, tayari Serikali imekwisha toa ruzuku hiyo katika Awamu
Mbili, ambapo katika Awamu ya Kwanza kwa mwaka wa fedha 2013/14,
Serikali ilitenga kiasi cha Dola Laki Tano (US $ 500,000), ambapo jumla
ya vikundi 11 vya wachimbaji vilinufaika na kila kikundi au mchimbaji
walipata kilipata wastani wa Dola Elfu Hamsini (US $ 50,000).
Akizungumzia ruzuku Awamu ya Pili
alieleza kuwa, kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitenga takriban
shilingi Bilioni 7.2, ambapo wanufaika 111 walishinda kati ya waombaji
720.
“Waombaji wanatakiwa kuwasilisha
maombi yao ndani ya siku 21 kuanzia tarehe 20 Julai, 2016. Mwombaji
anatakiwa kujaza nakala Tatu (3) za fomu za maombi na kuziwasilisha
katika Ofisi ya madini ambapo wahusika wanafanya shughuli zao,” alisema
Prof. Mdoe.
Pia alizitaja nyaraka ambazo
mwombaji anatakiwa kuambatisha na maombi yake kuwa ni pamoja na; Nakala
ya leseni ya uchimbaji au biashara ya madini au leseni ya biashara
iliyothibitishwa na Kamishna wa viapo; Nakala ya Cheti na Katiba ya
kuandikishwa kwa kampuni au ushirika.
Aidha, alisema nyaraka nyingine
ni pamoja na Nakala za stakabadhi za malipo ya Serikali ya ada za mwaka,
mrabaha na kodi; Nakala ya Cheti cha Mlipa Kodi (TIN); Mpango wa
Utunzaji Mazingira (EPP) ulioidhinishwa na Afisa Madini Kanda ikiwemo
taarifa ya uzalishaji kwa kipindi kisichopungua miezi sita.
Yapo mafanikio ambayo
yamepatikana kufuatia Serikali kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo.
Baadhi ya mafanikio ya wanufaika wa ruzuku Awamu ya kwanza ni pamoja na
Kikundi cha Itandura Miners Cooperation Society cha Nyamongo
kilichoongeza uzalishaji wa dhahabu, kampuni ya Precious Decor ya Tanga
inayomilikiwa na Mwanamama inayochimba madini ya stone ambayo sasa ni
maarufu jijini Dar Es Salaam kwa kurembesha kuta .
Aidha, mbali na utoaji ruzuku,
Serikali imefanya jitihada kadhaa za kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa
madini na kuhakikisha kuwa, uchimbaji mdogo unakuwa endelevu na unakua
kutoka uchimbaji mdogo kwenda uchimbaji wa Kati hatimaye mkubwa.
Kufuatia malengo hayo, tayari
Serikali imetenga maeneo 35 kwa wachimbaji wadogo yenye jumla ya hekta
242,400.81 sehemu mbalimbali Tanzania Bara.
Pia, Serikali imepanga kujenga
vituo saba vya mfano katika maeneo ambayo kuna uchimbaji mwingi wa
madini, ambapo vituo hivyo vinatarajiwa kujengwa kati ya mwaka 2016 hadi
2018. Aidha, vituo hivyo, vitaitwa centres of excellence ambapo
migodi ya mfano itajengwa na mitambo ya uchenjuaji itasimikwa ili
wachimbaji wapate huduma ya kuchenjuliwa madini yao kwa gharama nafuu.
Aidha, ili kuhakikisha madini ya
vito yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani, Serikali imefungua Kituo
cha mafunzo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kilichopo Mkoani Arusha kwa
ajili ya kufundisha uchongaji na ukataji wa madini hayo ili kuyaongezea
thamani.
Pia, Serikali kupitia Shirika
la Madini la Taifa (STAMICO), linatoa huduma ya mafunzo ya kitaalamu ya
nadharia na vitendo kwa wachimbaji wadogo wa madini na kuwapatia
miongozo ili kuboresha shughuli zao.
Miradi inayoweza kupewa ruzuku katika awamu ya III ni kama ifuatavyo:
NA | AINA YA MIRADI | KIWANGO CHA JUU CHA RUZUKU (USD) |
1 | Miradi ya kuendeleza, kuboresha na kupanua uchimbaji madini au kurekebisha mazingira yaliyotokana na shughuli hizo. | 100,000 |
2 | Miradi ya kupanua na kuboresha uchenjuaji madini au kurekebisha mazingira yaliyotokana na shughuli hizo. | 100,000 |
3 | Miradi ya kuboresha teknolojia ya uchimbaji madini, uongezaji thamani au uchenjuaji usiotumia zebaki. | 100,000 |
4 | Miradi ya uongezaji thamani hususani ukataji na uchongaji madini / mawe. | 100,000 |
5 | Miradi ya wakina mama katika maeneo ya uchimbaji mdogo yenye lengo la kutoa huduma kwa wachimbaji wadogo. | 15,000 |
0 maoni:
Chapisha Maoni