Posted by Esta Malibiche on Nov 3,2016 in NEWS
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, Serikali imekwishapeleka zaidi ya
sh. bilioni 177 kwenye halmashauri mbalimbali nchini ili kutekeleza
miradi ya maendeleo.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Novemba 3, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa
na Mbunge wa Viti Maalumu, Bibi Munde Tambwe aliyetaka kupata kauli ya
Serikali kuhusu ucheleweshwaji wa fedha za bajeti ya maendeleo katika
halmashauri mbalimbali nchini.
“Kwa kuwa Serikali ina mifumo,
miongozo, sheria na taratibu za kupeleka fedha kwenye halmashauri mara
baada ya kikao cha bajeti. Mheshimiwa Waziri Mkuu unatoa kauli gani
kuhusu ucheleweshwaji wa fedha hizo katika halmashauri nchini zikiwemo
za mkoa wa Tabora? Alihoji Mheshimiwa Munde.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu
amesema: “Baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi ya
fedha, Serikali ilianza kujiridhisha uwepo wa mfumo sahihi ya makusanyo
na mapato na matumizi yake. Ni kweli kwamba Serikali yetu baada ya
kikao cha bajeti inawajibika kutekeleza maamuzi ya Bunge kwa kupeleka
fedha zilizopangwa.”
Waziri Mkuu amesema Serikali
ilianza kupeleka watumishi watakaosimamia ukusanyaji mapato katika
halmashauri zote nchini. Kutathmini miradi yote iliyoanza ambayo
haijaendelezwa pamoja na mipya ili kutambua thamani na kisha kupeleka
fedha.
Amesema Serikali itaendelea na
upelekaji wa fedha kwenye halmashauri kwa ajili ya utekelezaji wa
shughuli za maendeleo. Amezisisitiza halmashauri hizo kuendelea
kukusanya mapato ndani ili kuongezea bajeti kwa fedha wanazopelekewa na
watumie mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti mapato hayo.
Aidha, Waziri Mkuu amezitaka
halmashauri zote nchini zihakikishe fedha zinazopelekwa katika maeneo
yao zinatumika kama ilivyokusudiwa kwa miradi husuka. Amewasihi Wabunge
wafuatilie na wasimamie matumizi ya fedha hizo ili miradi iliyopangwa
iweze kukamilika.
Wakati huo huo; Waziri Mkuu
amesema Serikali haijafilisika na kuhusu suala la mfuko wa jimbo bado
unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na wabunge watajulishwa
kiasi kilichopelekwa ili waweze kuratibu miradi yao ya maedndeleo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo
wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Ukonga Mheshimiwa Mwita
Waitara aliyetaka kupatiwa kauli ya Serikali kuhusu kutopelekwa kwa
fedha za mfuko wa jimbo.
Pia Mheshimiwa Waitara
alilalamikia kitendo cha jimbo lake kutengewa fedha kidogo katika mgawo
wa mfuko wa jimbo ambazo ni sh. milioni 16 licha ya kuwa na wananchi
wengi huku jimbo la Segerea alilosemma lina watu wachache likitengewa
sh. milioni 33. Ameiomba Serikali ingalie upya ugawaji huo kulingana na
mazingira ya jimbo husika.
Waziri Mkuu amesema kumejitokeza
matatizo kwenye halmashauri zenye majimbo zaidi ya moja na Serikali
inaendelea kufanya sensa kutambua idadi ya wananchi kwenye majimbo hayo
ili itakapopeleka fedha iweze kuzingatia idadi hiyo na kuwawezesha
wabunge kupanga miradi ya maendeleo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, OKTOBA 3, 2016
0 maoni:
Chapisha Maoni