Posted by Esta Malibiche on Nov 8,2016 in NEWS
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais TAMISEMI Mhe.Suleiman Jafo akijibu hoja mbalimbali kutoka kwa
wabunge wakati wa kikao cha sita cha mkutano wa tano wa Bunge la 11
linaloendelea Mjini Dodoma Novemba 8, 2016.
…………………………………………………………………….
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.
Jumla ya madereva 62 wanaoendesha
mabasi yaendayo haraka (UDART) wamechukuliwa hatua za kinidhamu kwa
sababu ya kukiuka Sheria za barabarani.
Idadi hiyo ya madereva imetajwa
leo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe Suleimani
Jafo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kiembe Samaki Mhe. Ibrahim
Mohammed lililohoji kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali juu ya
madereva hao ambao hawafuati sheria za barabarani.
Mhe. Jafo amekiri kuwa madereva
hao wamekuwa wakiendesha mabasi hayo kwa kasi kubwa kiasi cha
kuhatarisha maisha ya watu waendao kwa miguu lakini madereva hao
wanapaswa kuzingatia Sheria za usalama barabarani kama ilivyo kwa
madereva wanaoendesha aina nyingine ya magari.
“Tangu mabasi haya yaanze kutoa
huduma, tumeshawachukulia hatua za kinidhamu madereva 62 ambapo kati ya
hao, madereva 20 wamepewa onyo kwa makosa ya usalama barabarani, wawili
wamefukuzwa kazi na madereva 40 wamekatwa mishahara yao kwa makosa
mbalimbali ya barabarani”, alisema Mhe. Jafo.
Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa
kwa sasa mabasi hayo yamefungwa vifaa maalum kwa ajili ya kutoa ishara
ya dereva anayezidisha mwendo wa zaidi ya Kilomita 50 kwa saa moja ili
kudhibiti mwendo mbaya wa mabasi hayo.
Aidha, ili kuwakumbusha taratibu
na maadili ya kazi ya udereva Mhe. Jafo ameeleza kuwa Serikali imeweka
utaratibu wa kuwajengea uwezo madereva hao kupitia semina zinazoendeshwa
na wataalam kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha
Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) pamoja na Askari wa Usalama
Barabarani.
Amefafanua kuwa watoa huduma
wanatakiwa kuzingatia muda katika kutoa huduma mkataba baina ya DART na
mtoa huduma ambaye ni U- DART unaoainisha kuwa huduma ya mabasi yaendayo
haraka itaanza kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi sa 06:00 usiku.
0 maoni:
Chapisha Maoni