Jumatano, 16 Novemba 2016

Qatar Airways yaunga mkono jitihada za Rais Magufuli kwa kutoa madawati Kisarawe


Katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kumaliza tatizo la madawati mashuleni, Shirika la ndege linalotoa huduma ya usafirishaji wa anga la Qatar Airways nchini Tanzania limechangia msaada wa madawati 100  kwa Shule ya Msingi ya Chanzige B, iliyopo  Kisarawe mkoani Pwani.
Msaada huo wa Qatar Airways  ni sehemu ya mradi wa kusadia juhudi za Serikali kupitia mpango wa kuondoa uhaba wa Madawati nchini hasa shule za msingi ambapo pia  kwa shirika hilo imefanya hivyo kama moja ya kurudisha shukrani kwa jamii.
Akipokea madawati hayo 100, Mbunge wa Kisarawe na Naibu Waziri wa ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mh.Suleiman  Jafo ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo,  ameshukuru kwa msaada huo kwani umewezesha kupunguza kero kwa wanafunzi waliokuwa wakikaa chini  huku akiomba uongozi wa shule hiyo kuangalia uwezekano wa kugawa madawati hayo shule jirani pale wanapoona panafaa kutokana na uhitaji uliopo.
Aidha, Mh. Jafo ameliomba Shirika hilo la  Qatar Airways kuangalia  uwezekano wa kupiga tafu shule ikiwemo huduma zingine ikiwemo ujenzi wa Maktaba kama watakuwa tayari kwani tayari shule ina eneo la uwanja mkubwa wa ujenzi huo.
“Sisi watanzania. Tunafarijika na utendaji wenu  Qatar Airways wa kazi hapa nchini Tanzania. Ndio maana sasa hivi tunaboresha miundombinu ya uwanja wetu wa ndege hapa nchini. Tunaamini kupitia ndege zenu tutapata watalii mbalimbali ambao watakuwa chachu ya uchumi wa Tanzania” alieleza Mh. Jafo.
Kwa upande wake  Meneja wa Qatar airways Tanzania, Bw. Basek Haydar ameeleza kuwa, wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuchangia huduma za kijamii pamoja na kuimalisha usafiri wa anga  kwa kuwa na safari zake mbalimbali kutokea hapa nchini Tanzania.
Tukio hilo limefanyika Novemba 14.2016 katika viwanja vya shule hiyo ya Chanzige B,  ambapo pia viongozi  mbalimbali walihudhuria  wakkiwemo wafanyakazi wa Qatar na wawakiishi kutoka ofisi ya Doha pamoja na Dk. Amon Mkoga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Amon Mkoga Foundation, bodi ya wakurugenzi, walimu wa shule hiyo, wazazi na wanafunzi.

0 maoni:

Chapisha Maoni