Posted by Esta Malibiche on Nov 20,2016 in NEWS
Mhe Ummy akiongoza kikao cha
Mawaziri wa Afya wa Afrika Mashariki. Kulia kwake ni Mhe Christophe
Bazivamo Naibu Katibu Mkuu wa EAC…na kulia ni Dr Kwessi akimwakilisha
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Tanzania
…………………………………………………………………
NA MWANDISHI WETU – NAIROBI
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameongoza kikao cha mkutano
wa 13 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya wa nchi za Afrika
Mashariki.
Mkutano huo ulifanyika juzi jijini Nairobi, Kenya ambapo pia ulijadili masuala mbalimbali yahusuyo sekta ya afya kwa ujumla.
Katika taarifa yake aliyoituma
kwa vyombo vya habari, Waziri Ummy alisema mkutano huo ulihudhuriwa na
Mawaziri wa Afya wa Kenya, Burundi, Uganda pamoja na Mwakilishi wa
Waziri wa Afya wa Rwanda.
“Mkutano huo ulitanguliwa na
kikao cha wataalam na kikao cha makatibu wakuu wa wizara za afya katika
nchi wanachama vilifanyika kuanzia Novemba 14 hadi 17, mwaka huu,”
alisema.
Alisema mambo makubwa
yaliyojadiliwa na kupitishwa katika mkutano huo ni Sera ya Afya ya EAC
(EAC Regional Health Policy) na Sera, Mwongozo na Mkakati wa EAC wa Afya
ya Mama, Mtoto na Vijana (Intergrated EAC Reproductive, Maternal,
Newborn, Child and Adolescent Health Policy Guidelines and Strategic
Plan).
“Sera hizi zitasimamia
utekelezaji wa mipango ya kuboresha na kuimarisha afya katika nchi
wanachama wa Jumuiya kwa utaratibu unaofanana,” alisema.
Waziri Ummy alisema mkutano huo
wa Mawaziri pia ulichambua na kupitia taarifa ya Makatibu Wakuu wa
Wizara za Afya ambapo ulieleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika
utekelezaji wa maagizo ya mawaziri wa afya ikiwemo kuanzishwa kwa mpango
wa pamoja wa kusimamia dawa, mpango wa pamoja wa kukagua Vyuo Vikuu vya
Afya pamoja na mpango wa pamoja wa huduma za UKIMWI/VVU.
“Taarifa ya Ukaguzi wa Vyuo
Vikuu vya Afya vya Tanzania itawasilishwa katika Kikao cha 14 cha
Mawaziri wa Afya wa EAC kitakachofanyika Bujumbura Machi, mwakani,”
alisema.
Aliwashukuru Mawaziri wa Afya
wa Afrika Mashariki kwa kuendelea kusimamia vyema utekelezaji wa sera na
mipango ya kuboresha na kuimarisha huduma za afya ktk nchi zao.
Aliwataka kutekeleza maamuzi
waliyokubaliana katika Mkutano huu ili kutimiza kwa vitendo matarajio ya
wananchi wa Afrika Mashariki ya kuwa na Afya bora.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya la EAC hufanyika mara mbili kwa mwaka.
Lengo la Mkutano huu ni
kujadili utekelezaji wa sera, mipango na mikakati mbalimbali ya
kuboresha huduma za afya kwa nchi za Afrika Mashariki
0 maoni:
Chapisha Maoni