Posted by Esta Malibiche on Nov 8,2016 in BIASHARA
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akizungumza na Balozi wa Uingereza nchini, Mheshimiwa Sarah Cooke,
ofisini kwake bungeni mjini Dodoma Novemba 8, 2016. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu)
…………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameiomba Serikali ya Uingereza ihamasishe wawekezaji zaidi kutoka nchini
humo ili waje kuwekeza kwenye sekta ya viwanda.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne,
Novemba 8, 2016) wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini,
Bibi Sarah Cooke alipokutana naye ofisini kwake Bungeni, mjini Dodoma.
“Mheshimiwa Balozi utusaidie
kualika wawekezaji wengi zaidi kwenye maeneo ya kilimo, viwanda vya
usindikaji mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji, sekta ya mafuta na
gesi, nishati na ujenzi wa makazi hasa kwa mkoa wa Dodoma ambako hivi
sasa ni Makao Makuu ya Serikali,” amesema.
Amemweleza Balozi huyo kwamba
Tanzania imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati na hivyo imejipanga
kuwa na viwanda vya kutosha ili iweze kusindika mazao yake hapa nchini
na itoe ajira kwa wananchi wake.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
pia kuishukuru Serikali ya Uingereza kwa msaada wake mkubwa wa ujenzi wa
nyumba za walimu na shule mkoani Kagera zilizoathiriwa na tetemeko la
ardhi lilitokea Septemba 10, mwaka huu.
Kwa upande wake, Balozi Cooke
ambaye alifika kujitambulisha rasmi, amesema ameguswa na juhudi
zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na masuala ya ufisadi na
rushwa. “Kaulimbiu yenu kwamba rushwa haikubaliki (zero tolerance on
corruption) inaonyesha jinsi mlivyodhamiria kupambana na baa hili,”
amesema.
Amesema Uingereza inaongoza
miongoni mwa nchi zenye wawekezaji wengi hapa nchini na kwamba
inaendeleza mpango wake wa uwekezaji ambao unalenga maeneo makuu manne
ambayo ni gesi na mafuta; kilimo; nishati jadidifu na uimarishwaji wa
mazingira ya kufanya biashara.
Balozi Cooke alitumia fursa hiyo
kutoa pole kwa Serikali kutokana na msiba wa Spika Mstaafu wa Bunge la
Tisa na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Urambo, Tabora, Mheshimiwa Samwel
Sitta kilichotokea usiku wa kuamkia Novemba 7, mwaka huu katika
hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani alikokuwa
akipatiwa matibabu.
0 maoni:
Chapisha Maoni