Posted by Esta Malibiche on Nov in MICHEZO
UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika
Mashariki na Kati Azam FC, unayofuraha kuwaataarifu wapenzi wa soka kuwa
jioni ya leo umefanikiwa kuingia mkataba wa miaka mitatu na kiungo
mshambuliaji kutoka Ghana, Enock Atta Agyei.
Agosti mwaka huu, Azam FC
tuliingia makubaliano maalumu na Medeama ya Ghana juu ya kumsajili kinda
huyo anayetimiza umri wa miaka 18 mwakani baada ya benchi la ufundi
kuridhishwa na uwezo wake na sasa amejiunga rasmi kwenye viunga vya Azam
Complex.
Agyei anasaini mkataba tayari
kabisa kuanza kuitumikia Azam FC katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL) mwakani pamoja na michuano mingine ikiwemo
Kombe la Shirikisho Afrika.
Tunaamini ya kuwa ujio wa nyota
huyo wa timu ya Taifa ya Vijana ya Ghana chini ya miaka 17, utazidi
kuipa nguvu timu yetu kuelekea kwenye michuano inayotukabili mbeleni,
hivyo tunapenda kumtakia mafanikio mema kwa kipindi chote atakachokuwa
akiipigania jezi ya Azam FC.
Azam FC tunapenda kuwafahamisha
mashabiki wetu kuwa tutaendelea kukifanyia marekebisho kikosi chetu
kuelekea usajili wa dirisha dogo, lengo ni kukipa nguvu kikosi hicho ili
kifanye vizuri zaidi katika michuano ya hapa nchini pamoja na ile ya
Kimataifa.
Lengo kubwa la Azam FC ni
kuendelea kuwafurahisha mashabiki wetu kwa kupata matokeo bora uwanjani,
na tunaamini ya kuwa, benchi zuri la ufundi tulilokuwa nalo, wachezaji
wazuri walioko kikosini na wengine watakaokuja kuongeza nguvu, wote kwa
pamoja wataweza kutuvusha kuelekea safari ya mafanikio msimu huu.
Hivyo, tunawaomba mashabiki wetu
kuvuta subira na kuendelea kuisapoti timu kwani tunaamini ya kuwa nyie
ndio nguzo muhimu ya 12 uwanjani katika kuwapa hamasa wachezaji ya
kupata matokeo bora pamoja na kuijenga timu kiujumla.
Wakati huo huo, leo tumewapokea
wachezaji saba waliokuja kwenye majaribio ya kujiunga na Azam FC, ambao
ni mabeki wa kati Mbimbe Aaron Nkot (Cameroon), Kone Nabil Ibrahim
(Ivory Coast), kiungo mkabaji Kingue Mpondo Stephane (Cameroon),
Wengine ni washambuliaji Yaya Awaba Joel (Cameroon), Samuel Afful, Benard Ofori (wote Ghana) na Konan Oussou kutoka Ivory Coast.
0 maoni:
Chapisha Maoni