Posted by Esta Malibiche in Nov 15,2016 in NEWS
Na Juma Mohammed, Zanzibar
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed
Shein amesaini Mswada wa sheria ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na
gesi asilia na kusisitiza kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania haikuvunjwa.
Akizungumza
Ikulu Mjini Zanzibar jana wakati akitia saini Mswada wa sheria ya
utafutaji, uchimbaji wa mafuta na gesi asilia wa mwaka 2016, Rais Dk.
Shein alisema kwamba taratibu zote zimefuatwa wakati wa mchakato wa
kutunga kwa sheria hiyo na kuwaomba wananchi kuwapuuza wanaoeneza
uzushi.
Rais
Dk. Shein alisema haja ya kuwepo kwa sheria hiyo inatokana na masharti
ya kifungu cha nne Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia 2015 ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambayo inataja kwamba shughuli za uendeshaji wa
Mafuta na Gesi Asilia utafanywa Zanzibar kwa kusimamia na kuendeshwa na
taasisi kwa mujibu wa Sheria za Zanzibar.
“Kumekuwa
na maneno mengi kwamba nisisaini sheria hii, Hakuna katiba wala sheria
iliyovunjwa na tunawaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu, kuheshimu
sheria na kudumisha amani na mshikamano” Alisisitiza Rais Dk. Shein.
Rais
Dk. Shein amewataka wananchi wasikubali kuyumbishwa na wala
wasibabaishwe na watu wasioitakia mema Zanzibar. Alisema kwamba sheria
hiyo sasa itafungua milango kwa Makampuni mbalimbali kujitokeza kuanza
kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asili Visiwani
Zanzibar.
Alisema
kwamba kuna kazi kubwa ya kufanya katika utafutaji na uchimbaji wa
mafuta na gesi asilia hivyo amewaomba wananchi kuwa wavumilivu na kutoa
ushirikiano katika shughuli hiyo ambapo pia amewataka wataalamu katika
fani ya mafuta kufanyakazi kwa bidii na maarifa zaidi.
Rais
Dk. Shein alisema hadi sasa kuna Makampuni mawili yamejitokeza kuomba
kuwekeza katika kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia
Zanzibar akiyataja makampuni hayo kuwa ni Ras Gas ya Ras Al –Khaimah na
shell.
Rais
Dk Shein alisema baada ya mazungumzo ya Serikali mbili katika usimamizi
wa rasilmali za Mafuta na Gesi Asilia, iliamuliwa kuwa kila upande
katika Jamhuri ya Muungano upewe uwezo wa kusimamia rasilmali hizo na
kuanza kwa kufutwa kwa Sheria ya Jamhuri ya Muungano ya Sheria ya Mafuta
ya mwaka 1980 na kuanzishwa kwa Sheria mpya ya Mafuta ya mwaka 2015
ambayo ilijengeka katika misingi ya usimamizi wa rasilmali za mafuta na
gesi kwa Tanzania Bara.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo ilitakiwa kuanzisha sheria yake
yenyewe ambayo itasimamia Shughuli kama hizo kwa Zanzibar. Katika
kutumia nafasi hiyo, SMZ ilianza kuchukuwa hatua za kuelimisha wadau
mbalimbali ndani ya Serikali kwa nia ya kujijenga uwezo ili kuanza
kujenga mazingira yakayo weza kuifanya Zanzibar kusimamia masuala ya
mafuta na gesi asilia.
Rais
Dk Shein alisema katika kipindi cha mwaka 2015 na 2016, Zanzibar
ilifanikiwa kuanza na matayarisho ya Sera ya Mafuta na Gesi na Sheria ya
Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia kwa kutumia wataalamu
wake wa ndani kwa kushirikisha ngazi mbalimbali za Serikali na wananchi
hususan Wawakilishi wa Wananchi.
Rais
Dk Shein alisema Mwezi Septemba 2016, Sera ya Mafuta na Gesi ambayo
ilisharidhiwa na Baraza la Mapinduzi ilikamilika na Baraza la
Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha rasmi Sheria ya Utafutaji na
Uchimbaji wa Mafuta ya Zanzibar ambayo leo nimeitia saini kuwa sheria
kwa kuanza kutumika.
0 maoni:
Chapisha Maoni