Posted by Esta Malibiche on Nov 20,2016 in NEWS
Waziri wa maliasili na
utalii,prof Jumanne Maghembe akizungumza katika mahafali ya sita ya chuo
cha utalii na hotel Njuweni,Kibaha mkoani Pwani(Picha na Mwamvua
Mwinyi)
…………………………………………………………………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WAZIRI wa maliasili na
utalii,Prof.Jumanne Maghembe, amesema sekta ya utalii kwasasa inachangia
dola bil.2 katika pato la Taifa kwa mwaka kutoka dola mil.800 iliyokuwa
ikichangia kipindi cha nyuma.
Aidha amesema serikali imeajiri
watanzania 500,000 moja kwa moja katika sekta hiyo ambapo wengine
mil.moja wamejiajiri wenyewe hali iliyosababisha kupunguza idadi kubwa
ya wahitimu kusota wakitafuta ajira hiyo.
Katika hatua nyingine,Prof.Maghembe amewataka wahitimu wa
masuala ya utalii nchini kutangaza vivutio vya Tanzania na kutoa huduma
bora wakati wanapopata ajira ili kuhamasisha watalii wa nje na kuongeza
pato la taifa.
Waziri huyo aliyasema hayo ,kwenye mahafali ya sita ya chuo cha
hotel na utalii cha Njuweni kilichopo mjini Kibaha,wakati alipokuwa
mgeni rasmi.
Alieleza kuwa sekta hiyo inakua
kwa kasi kimapato na kuongeza idadi ya watalii kila siku kwa asilimia
100 ukilinganisha na miaka kumi iliyopita.
Prof.Maghembe alisema ni matumaini yake miaka mitatu ijayo mapato yataongezeka mara tatu zaidi ya ilivyo sasa.
Aliwataka wahitimu kuacha
kujibweteka na elimu waliyoipata bali waendelee kujifunza lugha
mbalimbali na mafunzo ya fani hiyo ili kuongeza taaluma zao.
“Kama hamtofanya hivyo mtapunguza
idadi ya watalii ,msibweteke tumieni elimu yenu mliyoipata ili kuvutia
watalii waendelee kuja Tanzania na kupeleka sifa kwenye nchi zao
kutokana na ukarimu ,mapokezi na utoaji wenu huduma” alisema
prof.Maghembe.
Nae mkurugenzi wa chuo hicho Saidi Mfinanga,alisema njuweni ni
kati ya vyuo vya mwanzo katika sekta ya hotel na utalii nchini na
imechangia kwa kiwango kikubwa sekta hiyo.
Alielezea kwamba kuanzia mwaka
2000 hadi 2015 chuo hicho kimetoa wahitimu 6,832 ambao wameingia katika
soko la ajira nchini, katika upande wa hotel yaani hotel management na
uongozaji watalii.
Saidi alisema mapema mwaka huu chuo kilipata nafasi ya kualikwa katika mashindano ya 14 ya mapishi duniani,yaliyoitwa(14th
international Istanbul gastronomy festival 2016)yaliyofanyika katika
jiji la instabul nchini Uturuki huku kati nchi 36 zilizoshiriki
ilishinda nafasi ya pili.
Aliwaomba wazazi kuchangamkia
fursa ya elimu wanayotoa kwa kupeleka watoto wao waliomaliza kidato cha
nne na cha sita na kukosa nafasi ya kuendelea na masomo.
Nae mlezi wa chuo hicho Yusuph
Mfinanga alisema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya upungufu wa
vifaa vya kisasa vya kuendesha masomo ya TEHAMA .
Alisema ili kuendana na ulimwengu
wa leo TEHAMA ni mhimili mkubwa katika kila eneo la kiutendaji ambapo
chuo kina mpango wa kuendesha kozi ndefu hadi kufikia diploma kwenye
ngazi hiyo.
Mfinanga alimuomba waziri huyo
kuwasaidia kupata msaada wa vifaa vipya kwa masomo hayo kwani chuo
kimedhamiria kutoa mafunzo kwa mtandao kwa kila mwanafunzi kutumia
komputa yake .
Mkuu wa chuo hicho Nditi Rashid
alisema chuo cha njuweni kilianzishwa January 2000 kwa malengo ya kutoa
elimu ya utalii na hotel ili kuboresha huduma katika sekta hiyo nchini.
Alisema chuo hicho kwasasa ni
kikubwa ,lakini kilipo ni sehemu finyu kwa mahitaji ya sasa hivyo kuna
kilasababu ya kuongezwa ukubwa ili kukidhi mahitaji.
0 maoni:
Chapisha Maoni