Jumanne, 15 Novemba 2016

WAWILI WASHIKILIWA PWANI KWA KOSA LA KULIMA NA KUSAFIRISHA BANGI

Posted by Esta Malibiche on Nov 15,2016 in

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
JESHI la polisi mkoani Pwani linawashikilia watu wawili wanaodaiwa kuhusika na kilimo cha bangi kinyume na sheria huko kandokando ya bonde la mto Ruvu ambalo lipo ndani ya mkoa huo na Morogoro Vijijini eneo la Ngerengere.
Aidha jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine ambao walikimbia na kuacha makazi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia tukio hilo ,kamanda wa polisi mkoani Pwani,Boniventure Mushongi,alisema watu hao walitiwa nguvuni katika msako,ulioongozwa na mkuu wa polisi wilaya ya Kibaha SSP Mwenda,novemba 14 majira ya asubuhi kwenye bonde hilo na kubaini shamba la bangi lenye hekari tatu.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na Msahiro Msahiro(45)mkazi wa Usure Shuleni na Hamis selemani (38) mkazi wa Gwata.
Hata hivyo alieleza kuwa shamba hilo lilikuwa likitumiwa na watu hao kwa ajili ya kilimo cha zao hilo haramu la bangi kwa njia ya umwagiliaji ambapo waliliteketeza kwa moto.
Kamanda Mushongi alisema ,katika tukio hilo walifanikiwa pia kukamata magunia (mifuko ya sulphate)251 ikiwa na bangi kufuatia kufanyika  msako huo .
Kamanda huyo alibainisha, wamekamata mbegu za bangi zilizokuwa kwenye magunia 32,mashine za umwagiliaji sita(water pumps)pamoja na mipira yake.
Alifafanua kuwa wamekamata na pikipiki sita zilizokuwa zikitumiwa kusafirisha zao hilo haramu kutoka shambani kwenda kwenye masoko ya biashara hiyo.
“Haya ni madawa ya kulevya na sheria za nchi yetu hairuhusiwi kulima,kuuza wala kuyatumia ,sasa leo hii baadhi ya watu wanadiriki kuyalima na kuyasafirisha kupeleka kwenye masoko”
“Bangi linaharibu kwa kiasi kikubwa vijana wetu ambao ni nguvu kazi ya Taifa ,angalia,hekari hizi zote tatu,mbegu za bangi zikiingia mtaani zitaharibu afya na akili za vijana wangapi,”alisema kamanda Mushongi.
Kamanda Mushongi aliomba jamii kupiga vita aina zote za madawa ya kulevya ikiwemo bangi na kuwataka washirikiane na jeshi hilo kuwafichua wale wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Aliliomba kundi la vijana kuachana na tabia ya kukubali kushawishika ama kujiingiza katika vitendo vya kuvuta bangi na maadili yasiyo mema.
Kamanda Mushongi alisema bado wanaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na kikosi cha kupambana na dawa za kulevya ili kubaini wahusika wakuu na sheria ichukue mkondo wake.

0 maoni:

Chapisha Maoni